Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema kuwa hakuna atakayezuia mradi mkubwa wa bomba la mafuta Afrika mashariki, akipuuza azimio la wabunge wa Ulaya lililotaka mradi huo ucheleweshwe kutokana na lilichokiita ''ukiukwaji wa haki za binadamu''.
Kampuni ya Total Energies ya Ufaransa na shirika la Taifa la Mafuta la China zilitia saini makubaliano ya dola bilioni 10 mapema mwaka huu ili kuendeleza visima vya mafuta ya Uganda na kusafirisha mafuta hayo ghafi kupitia bomba la urefu wa kilomita 1,445 hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania kwenye bahari ya Hindi.
Mradi huo umekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na makundi ya mazingira ambayo yanasema unatishia maisha ya makumi kwa maelfu ya watu na mifumo dhaifu ya ikolojia katika eneo hilo.