Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mulamula: Hatupeleki majeshi Msumbiji

Ca4ebdbc8cbcad3255ff9c30537bc163.jpeg Mulamula: Hatupeleki majeshi Msumbiji

Thu, 27 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesisisitiza haja yake ya kushiriki mazungumzo ya kuimarisha ustawi wa amani na utulivu nchini Msumbiji kutokana na machafuko yaliyopo katika baadhi ya miji nchini humo.

Aidha, imezitaka jumuiya za kimataifa kuisaidia nchi hiyo kwa kupeleka misaada ya maendeleo huku ikisisitiza kuwa haina mpango wa kupeleka majeshi nchini humo kutokana na hali inayoendelea sasa.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati akifungua majadiliano ya wiki mbili na wadau kuhusu machafuko ya Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji yaliyoandaliwa na Kituo cha Sera za Kimataifa (CIP) na kufanyika Dar es Salaam.

Alisema majadiliano ya kulisaidia taifa hilo kutafuta amani ndicho kipaumbele cha Tanzania kwa kushirikiana na juhudi za taifa hilo kwa lengo la kukomesha vitendo vya uhalifu na ugaidi na kuimarisha amani, ulinzi na usalama.

“Kumekuwa na hali ya vikundi vya waasi vinavyofanya machafuko nchini Msumbiji na mtakumbuka tangu yalipoanza nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), zinakutana kutafuta suluhu,” alisema Balozi Mulamula.

Alisema kama ilivyo kawaida ya Tanzania inaumizwa na majanga ya mataifa mengine hivyo itaendelea kutia nguvu zake kuunga mkono juhudi za kuleta usalama.

Alisema Cabo Delgado ni mpakani na Tanzania ambako mikoa ya Mtwara na Ruvuma ipo karibu zaidi hivyo hali hiyo inatishia hata nchini ndio maana nchi inaungana kukabiliana na vitendo hivyo.

“Tanzania kama kawaida yetu amani ikihatarishwa katika nchi jirani sisi hatupati usingizi, tupo mstari mmoja kusaidiana na nchi za SADC kupambana na vitendo vya ugaidi,” alifafanua.

Alisisitiza katika majadiliano yao pamoja na kuangalia hali ya Msumbiji, wapanue wigo kuangalia masuala mtambuka yanayosababika kuvunjika kwa amani ikiwemo maendeleo duni.

Balozi Mulamula alisema umaskini ukizidi waasi hutumia mwanya huo kuwalaghai vijana waliokata tamaa kwamba athari za machafuko huwakumba zaidi wanawake na watoto.

Alizisisitiza nchi tajiri kuwa jawabu la changamoto hiyo lipo katika msaada utakaoinua maendeleo ya nchi hiyo na nyingine, na kutoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuunganisha nguvu kukabiliana na tatizo hilo kwani linahusu dunia kwa ujumla.

Alisema majadiliano hayo yatasaidia kutoa mchango wa mapendekezo, ya kuibua suluhu ya kudumu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CIP, Profesa Rwekaza Mukandala alisema mkusanyiko huo umefanyika kutokana na hali inayoendelea Msumbiji ukizingatia ni nchi jirani.

Alieleza kufurahishwa na msimamo wa serikali kuungana na nchi hiyo kujadili suluhu ya tatizo hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz