Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtuhumiwa wa Mauaji ya Watoto 12 Atoroka Mahabusu Kimaajabu

Mauaji Wanjala Wanjala

Wed, 13 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wiki kadhaa zilizopita, mitaa ya Jiji la Nairobi na viunga vyake ilizizima baada ya kukamatwa kwa Masten Wanjala, kijana ambaye alikiri kuhusika na mauaji mfululizo ya watoto yaliyokuwa yakiendelea katika jiji hilo.

Hata hivyo, siku moja kabla ya mtuhumiwa huyo kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya mauaji ya watoto hao, mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 20 ametoroka kutoka katika mahabusu iliyopo Kituo cha Polisi cha Jogoo Road katika mazingira yaliyojawa na utata na kuzusha hofu mpya.

Jeshi la polisi nchini Kenya likiongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi wa Jiji la Nairobi, James Mugera limethibitisha kutoroka kwa mtuhumiwa huyo na kueleza kwamba msako mkali unaendelea, huku likiwaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwake, wazitoe kwa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa polisi waliokuwa zamu katika kituo hicho, wanaeleza kwamba waligundua kwamba Wanjala ametoroka walipokuwa kwenye utaratibu wa kawaida wa kuhakiki mahabusu wote, Jumatano ya Oktoba 13, 2021 majira ya saa moja asubuhi ingawa bado hakuna anayeweza kueleza ametoroka katika mazingira gani.

Mtuhumiwa huyo, alitarajiwa kupandishwa kizimbani Oktoba 14, 2021 kuanza kusomewa mashtaka yake, baada ya ushahidi kuwa umekamilika ambapo mpaka sasa anatuhumiwa kwa mauaji mfululizo ya watoto zaidi ya 12, yaliyotokea katika Jiji la Nairobi, Machakos na maeneo kadhaa Magharibi mwa nchi hiyo.

Wanjala alikuwa chini ya kizuizi cha polisi kwa muda wa siku 30 wakati upelelezi wa kina ukiendelea kuhusiana na mashtaka hayo ya mauaji, ambapo kwa kinywa chake amekiri mbele ya polisi kwamba ni yeye ndiye aliyekuwa akihusika na wimbi la mauaji ya watoto, lililoitingisha Kenya kwa kipindi kirefu, na kueleza kwamba kabla ya kuwaua, alikuwa akiwanyonya damu.

Inaelezwa kwamba, huenda idadi ya watoto waliouawa na Wanjala, ikaongezeka na kufikia 13 hadi 14, ambapo wote ni wa kiume.

Awali, Wanjala baada ya kukamatwa alifikishwa katika Mahakama ya Makadara na kusomewa mashtaka yake mbele ya Jaji Angello Kithiji ambapo polisi waliomba muda wa siku 30 wa kuendelea kukaa na mtuhumiwa, ili kukamilisha ushahidi ambao ungetumika mahakamani.

Kijana huyo alikamatwa katikati ya Mwezi Julai, 2021 na amewaongoza polisi mpaka kwenye maeneo mbalimbali alikotendea unyama huo wa kuwaua watoto, huku pia akiwapeleka kwenye maeneo aliyokuwa akiitupa miili ya watoto hao baada ya mauaji.

Kilichozidi kuongeza hofu kwenye mioyo ya Wakenya wengi, ni baada ya mtuhumiwa huyo kukiri mbele ya polisi kwamba alikuwa akiwapa kirahisi watoto hao kwa kujifanya kuwa ni kocha wa soka la watoto, ambapo pia alieleza kwamba alikuwa akiwalewesha watoto hao kwa dawa za kulevya kabla ya kuwaua, huku wakati mwingine akinywa damu zao.

Kwa mujibu wa polisi, Wanjala alikamatwa kufuatia mauaji ya watoto wa wawili ambao miili yao ilitupwa nje kidogo ya Jiji la Nairobi ambapo baada ya uchunguzi, polisi waligundua kwamba watoto hao walikuwa wamenyonywa damu kabla ya kuuawa.

Upelelezi wa kina ukafanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambapo akiwa chini ya polisi, ndipo alipokiri kuhusika na mauaji ya watoto wengine zaidi ya kumi, na kuwapeleka polisi katika maeneo aliyokuwa akifanyia mauaji hayo na kuitupa miili ya watoto hao, ambao wengi walikuwa na umri wa kati ya miaka 12 hadi 14.

Kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kulizuka wimbi la watoto kupotea jijini Nairobi na maeneo ya jirani, ambao wengi wao walikuwa wakipatikana siku kadhaa baadaye, wakiwa wameuawa, jambo lililosababisha sintofahamu kubwa kwa wakazi wa Jiji la Nairobi na maeneo ya jirani.

Kwa mujibu wa polisi, mauaji ya kwanza ya Wanjala, yalikuwa ni ya binti mwenye umri wa miaka 12 aliyetekwa kisha kuuawa miaka mitano iliyopita, katika kitongoji cha Machakos, Mashariki mwa Nairobi.

Huo ulikuwa mwanzo tu, baada ya hapo, mauaji yaliendelea huku mara kadhaa wananchi wenye hasira kali wakiwavamia na kuwachomea nyumba watu waliokuwa wakiwahisi kuhusika na mauaji hayo.

Taarifa zaidi za polisi, zinaeleza kwamba mara kadhaa, mtuhumiwa huyo alikuwa akiomba fidia kwa wazazi wa watoto aliowateka na iliposhindikana, alikuwa akiwaua kikatili na kuwatupa kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye mitaro ya maji machafu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live