Mmoja wa watoto wa kiume wa rais wa Equatorial Guinea, Ruslan Obiang Nsue, anayeshukiwa kuuza ndege kutoka shirika la ndege la kitaifa, amekamatwa na kuwekwa chini ya kizuizini.
Taarifa ya kukamatwa kwa Ruslan imetolewa na Kituo cha Luninga cha Serikali (TVGE), hii leo Januari 17, 2023 baada ya mwishoni mwa mwezi Novemba, mamlaka kufungua uchunguzi kufuatia kubainika kutoweka kwa ndege ya ATR 72-500 mali ya kampuni ya kitaifa”, Ceiba Intercontinental iliyokuwa katika ukarabati wa kawaida nchini Uhispania.
Obiang Nsue, anadaiwa kuweza kuuza ndege hiyo aina ya ATR kwa kampuni ya Binter Technic iliyobobea katika matengenezo ya ndege na yenye makao yake Las Palmas, kwenye kisiwa cha Uhispania cha Gran Canaria.
Ruslan Obiang Nsue, amewahi kuwa ni Katibu Waziri wa Michezo na Vijana, Mkurugenzi wa sasa wa Uwanja wa Ndege wa Ceiba, na awali alikuwa Naibu mkurugenzi wa Ceiba Intercontinental na kisha kuwa Meneja Mkuu na kaka yake ambaye ni Makamu wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue, aliyepewa jina la utani “Teodorin” ndiye ameamuru mdogo wake huyo akamatwe.
Teodorin Obiang mwenyewe alihukumiwa na mahakama ya Ufaransa mwishoni mwa mwezi Julai 2021 kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya euro milioni 30 na kutaifisha mali yake nchini Ufaransa kwa kuanzisha biashara ya kifahari nchini humo kwa njia ya udanganyifu.
Equatorial Guinea imetawaliwa kwa zaidi ya miaka 43 na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ambaye ndio kwanza amechaguliwa tena kwa muhula wa sita wa miaka saba na anashikilia rekodi ya dunia ya kukaa muda mrefu madarakani kwa mkuu wa nchi aliye hai, bila kujumuisha wafalme.
Pia nchi hiyo ni ya tatu kwa utajiri katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa Pato la Taifa kwa kila mtu mwaka 2021 kulingana na Benki ya Dunia, lakini iliorodheshwa ya 172 duniani kati ya 180 katika kipimo cha rushwa cha shirika la kimataifa la Transparency International.