Mtoto mkubwa wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni anasema atastaafu kutoka jeshini mwaka huu, baada ya kuhudumu kwa takriban miongo mitatu.
Muhoozi Kainerugaba, jenerali wa jeshi, alitoa tangazo hilo katika chapisho la Twitter.
"Nitastaafu UPDF mwaka huu," aliweka ujumbe huo kwenye Twitter.
Alitoa tangazo sawa na hilo kwenye Twitter mnamo Machi mwaka jana alipokuwa kamanda wa vikosi vya nchi kavu.
Lakini jeshi likasema halijapokea rasmi ombi la kustaafu la Bw Kainerugaba.
Matamshi yake ya hivi punde ya kustaafu yanakuja siku chache baada ya kufuta ujumbe wake wa Twitter akitangaza kuwa atagombea kiti cha urais mwaka wa 2026.
Jenerali huyo hajaficha nia yake ya kuchukua wadhifa huo wa juu kutoka kwa babake mwenye umri wa miaka 78, ambaye ameiongoza Uganda tangu 1986.
Sheria ya Uganda hairuhusu wanajeshi waliokazini kushiriki katika siasa.