Mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, Lt. Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kwamba kundi la waasi la M23, linalopigana vita na jeshi la serikali ya Kinshasa, lina haki ya kufanya hivyo.
Muhoozi ameandika ujumbe wa twiter akisema kwamba “ni hatari sana kwa mtu yeyote kupiga vita ndugu zetu. Sio magaidi, wanapigania haki za Watutsi wanaoishi DRC.”
Msimamo wa Generali Muhoozi ni tofauti na msimamo wa serikali ya Uganda ambayo imelazimika kutoa taarifa kupitia kwa msemaji wake Ofwono Opondo, kufuatia ripoti kwamba Uganda inaunga mkono wapiganaji wa M23.
Opondo alisema wiki hii kwamba “Uganda haiungi mkono kundi la waasi la M23” na kwamba “Uganda ina husiano mzuri sana na serikali ya Kinshasa katika kupigana na kundi la waasi la Allied democratic movement ADF.”
Raia wa DRC waliandamana mapema wiki hii, hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda, wakidai kwamba Uganda na Rwanda wanaunga mkono waasi wa M23, na kutaka mpaka kati ya DRC na nchi hizo mbili kufungwa.
Baadhi wa bunge na maseneta wa DRC vile vile walitaka DRC kufunga mpaka wake na Uganda, wakisema kwamba Uganda inaunga mkono makundi ya wapiganaji wanaoisumbua serikali ya Congo.
Akikutana na wajumbe wa umoja wa ulaya katika makao makuu ya jeshi la Uganda, Mbuya, karibu na Kampala, Alhamisi wiki hii, naibu kamanda wa jeshi la Uganda Generali Peter Elwelu, alisema kwamba “kundi la M23 linastahili kurudi katika sehemu zake ambazo lilikuwa linashikilia ili kuruhusu mazungumzo kufanyika.”
Ndege za kijeshi zimewasili Goma
Kenya imetangaza kwamba jeshi lake lipo tayari kuingia mashariki mwa DRC kwa ajili ya kupambana na makundi ya waasi.
Wanajeshi wa Burundi tayari wapo DRC kupambana na kundi la waasi la Red Tabara. Uganda inapambana na kundi la waasi la ADF.