Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania aliyeteuliwa bosi wa kodi Sudan Kusini afunguka

A10cf0c313ae5cf4f85e12aad3878244 Mtanzania aliyeteuliwa bosi wa kodi Sudan Kusini afunguka

Tue, 13 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MTANZANIA aliyeteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Taifa Sudan Kusini (NRA), Dk Patrick Mugoya, amesema uteuzi wake umetokana na utendaji kazi mkubwa aliofanya katika ukusanyaji mapato Tanzania.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa ajira hiyo mpya nchini Sudan Kusini juzi, alisema jukumu lake la kwanza litakuwa ni kutengeneza mpango mkakati wa kuwezesha uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato yasiyotokana na mafuta.

Dk Mugoya aliyewahi kuwa Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alisema pia atahakikisha NRA inafanya kazi kwa ufanisi, kujenga ushirikiano mzuri na wadau mbalimbali katika ukusanyaji wa mapato kwa uwazi, uwajibikaji na uhakika pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato kama vile ukwepaji kodi, misamaha ya kodi isiyo na tija na uingizaji bidhaa kinyemela.

“Kama mlivyoshuhudia tumemaliza kusaini mkataba wangu kama Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato ya Kitaifa, ninapaswa kukabiliana na vitu vitatu kwanza, tutafanya kazi kikamilifu kuhakikisha NRA inafanya kazi kwa ufanisi,” alisema.

Aidha, alisema atahakikisha NRA inashirikiana na wadau muhimu katika mpango mkakati wa mamlaka hiyo wa uhamasishaji ukusanyaji mapato yasiyo ya mafuta unaboreshwa kuwapo uwajibikaji.

“Wakati wa utekelezaji wa masuala hayo nitahakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato hauvurugwi. Tutafanya hatua hizi zote na wakati huohuo kuziba mianya na uvujaji wa mapato kwa wakwepa kodi, misamaha isiyo ya haki, kuzuia magendo na kadhalika kama hatua za haraka,” alisema.

Dk Mugoya alisema wataandaa mipango ya muda mrefu na kati kwa kushirikisha wadau wote.

"Hiyo inamaanisha wafanyikazi, uongozi wa mamlaka ya mapato, bodi yake, serikali, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia na wengine katika kupata mpango ambao utaleta mabadiliko,” alisema Dk Mugoya.

Katibu wa Kwanza katika Wizara ya Fedha Sudan Kusini, Garang Majak, alielezea matumaini yake kuwa Kamishna Mkuu huyo mpya wa NRA na timu yake watakusanya mapato mengi ili kukuza uchumi dhaifu wa Sudan Kusini.

"Tunajua kabisa kwamba tunakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, lakini timu mpya ya Kamishna na Naibu Kamishna wa NRA, Africano Mande, itahakikisha kunakuwa na mifumo ya kutosha na madhubuti ya kukusanya mapato ya kutosha,” alisema.

Majak alisema Sudan Kusini inaweza kukabiliana na tatizo la uchumi lililopo endapo mapato yote yatakusanywa vizuri na yatatumika kikamilifu katika kulipa mishahara, huduma za serikali pamoja na matumizi ya maendeleo.

Alitoa wito kwa washirika wa maendeleo kusaidia Sudan Kusini katika uhamasishaji na ukusanyaji mapato.

NRA ilianzishwa kama moja ya hatua za kupunguza utegemezi wa mapato ya mafuta, kuimarisha ukusanyaji mapato yasiyokuwa ya mafuta na kuimarisha udhibiti wa matumizi.

Dk Mugoya ambaye ni mchumi, amechukua nafasi ya Dk Olympio Attipoe aliyefukuzwa kazi Agosti, mwaka jana.

Akizungumzia kuteuliwa kwa Mtanzania huyo, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk John Mtui, alisema kumeonesha imani ya nchi hiyo kwa Watanzania hususan utendaji uliofanywa na serikali ya awamu ya tano katika ukusanyaji mapato.

Alimtaka Dk Mugoya kufanyakazi kwa uaminifu ili kuimarisha uchumi wa nchi hiyo jambo litakalosaidia kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania katika nyanja mbalimbali duniani.

Chanzo: habarileo.co.tz