Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtangamano EAC wakuna wabunge EALA

3b986db84fa196b337fa7a2e60bfd0d5 Mtangamano EAC wakuna wabunge EALA

Wed, 10 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WABUNGE wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wameridhishwa na hatua za mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unavyoendelea na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo.

Wakizungumza kuhusu miaka 22 ya mtangamano wa Afrika Mashariki na fursa zilizopo, Wabunge wa Tanzania wamehainisha mafanikio kadhaa yaliyopatikana na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zilizomo ndani ya jumuiya.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Adam Kimbisa alisema mtangamano wa EAC unatekelezwa katika hatua nne ambazo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na Shirikisho la Kisiasa.

Alisema katika Umoja wa Forodha baadhi ya masuala yaliyotekelezwa ni kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi wanachama kwa kuzingatia kanuni za uasili wa bidhaa, kuwa na wigo mmoja wa ushuru kwa bidhaa zinazotoka nchi moja kwenda nje ya jumuiya na kuanzishwa himaya moja ya forodha.

Alisema nyingine ni kuanzishwa kwa vituo vya pamoja vya utoaji wa huduma mipakani vya Rusumu, Namanga, Holili, Horohoro, Mutukula na Kabanga pamoja na sheria ya uzito wa magari ya EAC.

“Moja ya changamoto zinazokabili hatua hii ni uwapo wa vikwazo visivyo vya kiforodha na wananchi kutoelezwa suala zima la uasili wa bidhaa na jinsi ya kupata vibali vya kuonesha uasili wa bidhaa,” alisema Kimbisa.

Akizungumzia Soko la Pamoja, Mbunge huyo alisema wananchi wamekuwa huru kwenda mahali popote katika nchi wanachama, kuishi popote kwa ajili ya shughuli maalum, kufanya kazi mahali popote, uhuru wa kusafirisha mitaji na uwekezaji, uhuru wa kufanya biashara ya huduma na nyinginezo.

Hata hivyo, alisema kuna changamoto kadhaa ikiwamo kuchelewa kufanyika marekebisho ya sheria za nchi wananchama ili kufungua sekta zilizoainishwa katika itifaki ya Soko la Pamoja huku baadhi ya Watanzania kutopenda kutafuta fursa kwenye nchi nyingine kutokana na woga na kutopata taarifa sahihi.

Kuhusu Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki uliosainiwa 2013 na kuridhiwa na nchi zote, alisema wamekubaliana nchi zitakazoingia kwenye umoja huo ni zilizokidhi vigezo vya muungano wa uchumi vilivyowekwa, hivyo nchi zimepewa miaka 10 kuanzia mwaka 2014.

“Baada ya miaka 10 kama kutakuwa na angalau nchi tatu zilizokidhi vigezo basi Umoja wa Fedha utaanza kwa nchi zilizokidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei cha asilimia na deni la taifa lisizidi asilimia 50 ya pato la taifa na akiba ya fedha za kigeni isiyopungua mahitaji ya miezi minne na mengineyo,” alisema.

Alisema katika Shirikisho la Kisiasa, tayari kumeanzishwa Bunge la Afrika Mashariki, Mahakama ya Afrika Mashariki na kuimarishwa ushirikiano katika masuala ya usalama na katika sera za mambo ya nje, kutungwa kwa wimbo wa jumuiya na mengineyo.

Kimbisa alisema pia kuna Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Kamisheni ya Vyuo Vikuu ya EAC, Mamlaka ya Usimamizi wa Usalama na Usafiri wa Anga, Kamisheni ya Kiswahili, Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia, Kamisheni ya Utafiti wa Afya na Taasisi ya Uvuvi katika Ziwa Victoria zinazofanya kazi vema.

Wabunge wa EALA Kutoka Burundi, walisema kupungua kwa siku za kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kutoka siku 12 mpaka siku tatu kwa nchi zisizo na bandari ni mafanikio makubwa ndani ya Jumuiya.

Walisema ujenzi wa miundombinu umekuwa na manufaa makubwa kwa kujenga Bandari ya Kabanga, Kobero na Gasenyi -Nemba kwa ajili ya kukuza biashara, huku bidhaa zinazotoka Mombasa kwenda Burundi zilikuwa zikichukuwa siku 30 lakini sasa ni siku tatu.

Makamu wa Rais wa Wabunge wa EALA kutoka Burundi, Marie Mahirwa alisema kuna tatizo la muingiliano huru wa bidhaa, watu na mitaji na kwamba hali ni mbaya zaidi wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa corona kwani mipaka imefungwa na kuleta changamoto ya muingiliano wa jamii.

Nao wabunge wa EALA kutoka Kenya, wamezindua kampeni ya wiki moja kuhamaisha raia wa nchi hiyo kuhusu umuhimu wa mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Taarifa ya wabunge wa nchi hiyo iliyosomwa na Mbunge, Abdikadiri Aden ilisema lengo ni kukuza uelewa wa wananchi kuhusu EAC, umuhimu wake na changamoto zilizopo

Chanzo: www.habarileo.co.tz