Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msumbiji yateketeza kuku 45,000 kukwepa mafua ya ndege

Msumbiji Vifaranga Msumbiji yateketeza kuku 45,000 kukwepa mafua ya ndege

Sat, 21 Oct 2023 Chanzo: Mwananchi

Zaidi ya kuku 45,000 wamechinjwa, kuchomwa na kuzikwa Kusini mwa Msumbiji ili kuzuia kuenea kwa homa ya ndege, maafisa wamesema.

Kuku hao walikuwa wameagizwa kutoka nchi jirani ya Afrika Kusini, ambayo imekumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.

Mlipuko huo umeenea katika wilaya ya Morrumbene nchini humo katika jimbo la Kusini la Inhambane.

Mamlaka zinajaribu kuzuia ugonjwa huo huku hofu ikizidi kuenea katika maeneo mengine ya nchi.

Homa ya ndege ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huwapa viumbe jamii ya ndege.

Inaweza kuenea kwa makundi yote ya ndege ndani ya muda wa siku chache, kupitia kinyesi cha ndege na mate, au kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa.

Mlipuko huo umesababisha uhaba wa mayai na kuku, na kupanda kwa kasi kwa bei katika siku za hivi karibuni, nchini Msumbiji, ukiwemo mji mkuu Maputo.

Bei ya wastani ya kuku imeongezeka karibu mara mbili wakati bei ya mayai kadhaa imepanda kwa asilimia 50.

Kuku 45,000 walioteketezwa walikuwa wamegusana na kuku walioambukizwa na mafua ya ndege nchini Afrika Kusini, amesema Mkurugenzi wa Kitaifa wa Maendeleo ya Mifugo wa Msumbiji Américo da Conceição.

Kuku hao walikuwa wameletwa Msumbiji kutaga mayai.

Afrika Kusini imekuwa ikikabiliana na mlipuko mbaya zaidi wa mafua ya ndege, na kuwalazimu wafugaji wa kuku kuua kuku milioni saba wanaotaga mayai, ambayo ni sawa na asilimia 20-30 ya hifadhi nzima ya nchi hiyo, kulingana na Chama cha Kuku cha Afrika Kusini.

Mlipuko huo pia umesababisha uhaba wa usambazaji wa mayai na nyama ya kuku Msumbiji.

Da Conceicao amesema kuwa Msumbiji imepiga marufuku uingizaji wa kuku na bidhaa zao kutoka Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na mayai na chakula cha kuku.

Serikali pia imesitisha mzunguko wa kuku, mayai na chakula cha mifugo kutoka Morrumbene, kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo hadi maeneo mengine ya Msumbiji.

Mamlaka imesema kuku hao waliteketezwa ili kuzuia watu kuwachukua na kuwala baada ya kuchinjwa.

Chanzo: Mwananchi