Balozi wa Marekani nchini Kenya sasa ameweka wazi kuwa hakuna mahusiano baina ya msaada wa Marekani nchini Kenya na suala la mapenzi ya jinsia moja akisema kuwa nchi ya Marekani ina ufahamu wa msimamo wa Kenya kuhusu LGBTQ na ya kuwa Marekani inatambua haki za LGBTQ kama haki za kibinadamu.
Whitman alisema pia kuwa Marekani inaheshimu mtazamo wa Kenya kuhusu suala la mapenzi ya jinsia moja.
Tetesi zilizuka baada ya Mama taifa wa Marekani Dr. Jill Biden kuipa Kenya msaada wa shilingi bilioni 16 ili kupambana na baa la njaa nchini. Tetesi hizo zilizuka na kukisiwa kuwa msaada huo ulipeanwa ili Kenya ikubali kupitisha LGBTQ.
Balozi Whitman alisema licha ya tofauti hizo za kiitikadi Kenya na Marekani ina uhusiano ulio dhabiti wa kikazi na kwenye ngazi zingine.
"Serikali ya Kenya inajua mtazamo wa Marekani lakini pia tunaheshimu maoni yao kuhusu haki za LGBTQ. Hakuna uhusiano kamili kati ya chakula na misaada ya ukame na msimamo wa Wakenya kuhusu LGBTQ..."alisema Whitman.
Seneta wa Nandi pia Samson Cherargei alitetea serikali kwa kusisitiza kuwa hamna uhusiano wowote baina ya mambo hayo mawili akisema kuwa isitafsiriwe kuwa msaada huo wa serikali ya Marekani ilikuwa kutaka Kenya ihalalishe LGBTQ.
"Kuna madai kwamba Ksh. bilioni 15 ambazo zimetolewa kwa serikali kupambana na ukame zilikuwa kwa hisani ya kuunga mkono ushoga nchini... Nataka kukanusha kuwa si kweli," alisema.