Mhasibu wa Afrika Kusini aliyekuwa akichunguza kesi za ufisadi wa hali ya juu ameuawa kwa kupigwa risasi pamoja na mwanawe.
Cloete Murray mwenye umri wa miaka 50, alikuwa afisa anayekamilisha shughuli za kampuni iliyoporomoka ya Bosasa, iliyohusishwa na kashfa nyingi za kandarasi za serikali.
Pia alifanya kazi kama afisa anayeangazia masuala ya makampuni yanayohusishwa na ndugu tajiri wa Gupta, ambao wanakanusha tuhuma za rushwa.
Polisi watafuatilia kuona ikiwa kuna uhusiano kati ya mauaji ya Bw Murray na uchunguzi huu wa ufisadi.
Bw Murray alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa anaendesha gari mjini Johannesburg akiwa na mwanawe Thomas mwenye umri wa miaka 28, mshauri wa masuala ya sheria, siku ya Jumamosi.
Mwanaye alifariki katika eneo la tukio huku Bw Murray akipelekwa hospitalini na baadaye akafariki kutokana na majeraha aliyopata, vyombo vya habari viliripoti, vikimnukuu msemaji wa polisi.
Wawili hao walikuwa wakiendesha gari lao jeupe aina ya Toyota Prado kuelekea nyumbani kwao Pretoria, vyombo vya habari vya Afrika Kusini viliripoti.
Kazi ya Bw Murray kama mtu anayefuatilia masuala ya kampuni zilizoporomoka aliyeteuliwa na mahakama ilikuwa kuangalia akaunti za makampuni ambayo yalikuwa na dosari, kurejesha mali, na kuripoti uhalifu wowote.
Moja ya kampuni hizo ilikuwa Bosasa, mkandarasi wa serikali aliyebobea katika huduma za magereza.
Tume ya kihistoria ya Zondo kuhusu ufisadi ilihitimisha kampuni hiyo iliwahonga sana wanasiasa na maafisa wa serikali ili kupata kandarasi za serikali katika kipindi cha miaka tisa ya urais wa Jacob Zuma, kuanzia 2009 hadi 2018.
Bw Zuma alikataa kushirikiana na uchunguzi huo lakini amekanusha tuhuma za ufisadi. .
Mnamo mwaka 2018, Rais wa sasa wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema atalipa mchango wa $35,000 (£27,300) kutoka Bosasa.
Mpelelezi wa kupambana na ufisadi aligundua alidanganya bunge kuhusu mchango huo, lakini matokeo ya utafiti huo yalitupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.
Bw Ramaphosa pia amekabiliwa na madai mengine ya ufisadi, ambayo anakanusha.
Bosasa iliingia katika kazi ya kufuatilia kampuni zilizofilisika kwa kujitolea baada ya benki kufunga akaunti zake.