Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Morocco yasifu msimamo wa Nyerere umoja Afrika

4f0afe6786cc9a3d0c0d0bbfe913baf7 Morocco yasifu msimamo wa Nyerere umoja Afrika

Thu, 8 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MOROCCO imepongeza mtazamo wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere wa kutaka kuwapo na umoja kama Afrika inataka kusonga mbele kisiasa na kiuchumi.

Balozi wa Morocco nchini, Abdelilah Benryane alitoa pongezi hizo wakati akiwasilisha mada katika mhadhara unaohusu Mwalimu Nyerere kutaka umoja badala ya utengano miongoni mwa nchi za Afrika.

Wakati akiwasilisha mada Balozi Benryane alisema mafanikio ya falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kuhimiza umoja yameonekana kizazi hadi kizazi.

Alisema ni wakati muafaka kwa kila kiongozi wa Afrika kuweza kusimamia falsafa hizo na kuzitekeleza katika majukumu yao kwa kuwa ni moja ya nguzo ambayo itaendelea kuenziwa.

“Sio kila kiongozi alikuwa na karama ya kuunganisha taifa la Afrika, kwa kuwa wamoja kila mmoja amejua ni aina gani ya eneo alitakalo kama ni lenye kusimamia umoja ama la,” alisema Balozi Benryane na kuongeza kuwa viongozi wa Afrika wanatakiwa kutambua kuwa ipo nguvu na mamlaka katika taifa lenye umoja.

Alisema falsafa za Mwalimu Nyerere ikiwemo ya kuimarisha umoja imeweza kutoa suluhu kwa nchi zilizokuwa zikikabiliwa na migogoro, na kwa mantiki hiyo ipo haja kwa ndoto wa wazee waliotanguliwa kukumbukwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku alisema Mwalimu Nyerere alishirikiana na nchi nyingine ikiwemo Morocco kuhakikisha unaundwa umoja wa Afrika na kusaidiana kupigania uhuru wa bara la Afrika.

“Mwalimu ameshughulika na umoja wa Afrika na kuhakikisha kila nchi ijikomboe ikiwemo kisiasa, na Morocco walimheshimu sana Mwalimu na ndio maana hadi sasa MNF inasimamia na kuhimiza amani na umoja kwa maendeleo ya watu,” alisema.

Butiku alisema Nyerere alisimamia umoja ikiwa ni silaha ya kuimarisha uhuru na kujikomboa katika uchumi.

Alisema kwa kuzingatia hilo MNF imekuwa ikiwakutanisha waliohusika na amani na umoja ili wananchi wapate maendeleo na kuhakikisha kama zipo tofauti baina yao zinaondolewa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz