Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani uamuzi wa serikali ya Morocco wa kumkabidhi kwa viongozi ukoo wa Aal Saud, mwanaharakati wa Saudia anayetumia haki yake ya kueleza anachokiamini.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Tasnim ambalo limeyanukuu mashirika ya kutetea haki za binadamu yakilaani uamuzi wa mahakama ya Morocco kumkabidhi kwa viongozi wa Saudi Arabia, mwanaharakati Hassan al Rabie, licha ya onyo kwamba maisha yake yatakuwa hatarini.
Mashirika hayo yamemwandikia barua Waziri Mkuu wa Morocco, Aziz Akhannouch, yakilaani vikali uamuzi wa serikali ya Rabat wa kumrejesha al Rabie nchini Saudi Arabia.
Katika barua yao hiyo, imeelezwa kuwa Morocco ilimkabidhi mwanaharakati huyo wa Saudia kwa mamlaka ya Saudi Arabia tarehe 6 mwezi huu wa Februari.
Mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yamesisitiza pia kuwa al Rabie sasa anakabiliwa na hatari kubwa ya kuteswa na kujeruhiwa vibaya kutokana na sababu zinazohusiana na imani yake ya kidini na historia ya familia yake ya kushiriki katika maandamano ya kisiasa.
Hassan Muhammad al Rabie anatokea eneo la Qatif, na aliondoka nchini kwake kihalali mwaka mmoja na miezi miwili iliyopita na alikuwa njiani kuelekea nchini Oman, Indonesia na baadhi ya nchi nyingine. Safari yake ya mwisho nchini Morocco ilikuwa pale vikosi vya usalama vya nchi hii vilipomkamata. Alikaa Morocco kwa karibu miezi 5.