Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moi yafanya operesheni 27 za kichwa bila kufungua fuvu

8f13621c73ba027f1c0550144d1201d4 Moi yafanya operesheni 27 za kichwa bila kufungua fuvu

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAGONJWA 27 wamefanyiwa upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu la kichwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji huo katika maabara ya kisasa ya upasuaji ubongo bila kufungua fuvu la kichwa tangu ilipoanza kufanya kazi Januari 8, mwaka huu, ambapo serikali ilimetumia zaidi ya Sh bilioni 7.9 kuijenga.

Akizungumza juzi wakati wa ziara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima, Mkurugenzi wa MOI, Dk Respicious Boniface alisema taasisi hiyo imeendelea kusogeza huduma kwa wananchi ili kupunguzia adha kwa wagonjwa kusafiri kufuata huduma Dar es Salaam.

“Tumesogeza huduma za kibingwa za ubongo KCMC (Moshi) pamoja na Bugando (Mwanza), tumesogeza huduma za mifupa Hospiali ya Kanda Mbeya na Nyangao Lindi,” alisema Dk Boniface.

Kwa upande wake, Dk Gwajima aliipongeza MOI kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania kwa kipindi cha miaka 25.

“Hongereni mnafanya kazi nzuri, nimekuja hapa tujadiliane ili tuone ni namna gani MOI itafikisha miaka 30 ikiwa bora zaidi, kueni huru kuchangia mada ili tusonge mbele zaidi,” alisema.

Dk Gwajima pia alipokea maoni, michango pamoja na changamoto mbalimbali zinazolenga kuboresha hali ya utoaji huduma MOI.

Hata hivyo, aliipa siku 10 taasisi hiyo kuandaa taarifa itashughulikiaje changamoto zilizo ndani ya uwezo wao na kuziwasilisha kwake.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI, Profesa Charles Mkonyi alisema taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha kliniki katika wilaya za mkoa wa Dar es Salaam ili kuwasogezea huduma wananchi.

“Pamoja na kuanzisha hizi kliniki, pia tunalenga kujenga hospitali ya kisasa ya utengamao katika kiwanja cha MOI kilichopo Mbweni Mpiji, Dar es Salaam,”alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz