Kamishna wa Kitaifa wa Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini (SAPS), Jenerali Fannie Masemola amethibitisha kwa masikitiko kifo cha mmoja wa wachunguzi wa kesi ya kutoroka kwa Thabo Bester.
Polisi walisema wanachunguza mazingira ya tukio hilo la kujiua kwa Brigedia Jackson Mkhaulesi mwenye umri wa miaka 59. Alipatikana amefariki ndani ya gari lake siku ya Jumatatu.
Haya yanajiri baada ya mahakama kuu ya Free State kukataa ombi la Dkt Nandipha Magudumana la kutaka kukamatwa kwake na kupelekwa Afrika Kusini kutangazwa kuwa ni kinyume cha sheria. Mahakama ilitupilia mbali maombi yake huku akikubali kurejea Afrika Kusini.
Habari za kifo cha Brigedia Mkhaulesi zimeleta mshtuko nchini Afrika Kusini afisa wa upelelezi wa polisi aliyehudumu kwa miaka 31.
“Kwa miaka mingi amejidhihirisha kuwa ni mpelelezi mwenye ujuzi wa hali ya juu mwenye uzoefu na maarifa mengi katika kugundua uhalifu. Kuondoka kwake kunaacha pengo katika mazingira ya upelelezi wa SAPS. Kwa niaba ya SAPS, tunatoa pole kwa familia, marafiki. na wafanyakazi wenzetu”, alisema Jenerali Fannie Masemola.
Utambulisho wa marehemu utatolewa mara tu wanafamilia wake wote watakapoarifiwa.
Thabo Bester anajulikana kama “mbakaji wa Facebook” kwa kutumia tovuti za mitandao ya kijamii kuwarubuni waathiriwa wake. Alidanganya kufariki na kutoroka gerezani mwaka jana. Yeye na mpenzi wake, ambaye anatuhumiwa kumsaidia kutoroka, walikamatwa nchini Tanzania mwezi Aprili na kurejeshwa Afrika Kusini ili kujibu mashtaka.
Kesi dhidi ya Magudumana, Bester na washtakiwa wengine sita – Senohe Matsoara, Zolile Sekeleni, Teboho Lipholo, Motanyane Masukela, Tieho Makhotsa na Nastassja Jansen – iliahirishwa hadi Juni 20 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Bloemfontein kwa uchunguzi zaidi.