Maafisa wa afya Uganda wanachunguza mripuko wa ugonjwa usiojulikana ambao umewaua takriban watu kumi na wawili katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita katika wilaya ya Kyotera iliyoko katikati mwa Uganda.
Waathiriwa wa ugonjwa huo wanatokea vipele mwilini ambavyo vinasambaa na kuwa vidonda kabla ya kufariki dunia baada ya kuugua kwa siku chache huku wengine wakionesha dalili za kuvimba viungo vya mwili.
Wizara ya afya Uganda imechukua sampuli ya ngozi ya mmoja wa wagonjwa aliyefariki ili kufanyia vipimo.
Matokeo yake bado hayajatangazwa kwa umma.
Maafisa wa afya wa eneo hilo wanaonya kuwa imekuwa vigumu kudhibiti hali kwani baadhi ya wagonjwa wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji badala ya kwenda hospitali.