Takribani watu 23 wamekufa katika mlipuko mpya wa kipindupindu ambao ulikumba jamii zilizohamishwa na mafuriko ya hivi karibuni mashariki mwa Ethiopia, shirika la hisani la Save the Children linasema.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi shirika la kutoa misaada lenye makao yake makuu nchini Uingereza limesema zaidi ya wagonjwa wa kipindupindu wamethibitishwa katika muda wa wiki mbili pekee katika eneo la Somalia, eneo lililoathiriwa zaidi na mafuriko ya hivi karibuni na mvua kubwa isiyo ya kawaida.
Mvua hiyo imewaathiri watu milioni 1.5 kote nchini huku idadi ya watu waliolazimika kuacha makazi yao ikifikia 600,000, UN ilisema.
Lakini ni asilimia 10 tu ya walioathirika kwa sasa wanapokea misaada huku Ethiopia ikiendelea kukabiliwa na mapungufu katika ufadhili, iliongeza.
Zaidi ya wilaya 90 nchini Ethiopia zimeripoti matukio ya ugonjwa wa kipindupindu huku shirika la Save the Children likionya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwani mvua nyingi zinatarajiwa kunyesha katika takribani mikoa mitatu.
Mvua kubwa iliyonyesha Ethiopia, pamoja na Somalia na Kenya, imesababishwa na hali ya hewa ya El NiƱo pamoja na nyingine inayojulikana kama Dipole ya Bahari ya Hindi.