Ulinzi umeimarishwa kati ya wasafiri wa ndani, wanaotoka na kuingia nchini Uganda ikiwa ni hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya nchi hiyo katika kuzuia virusi vya ugonjwa wa Ebola kusambaa ndani na nje ya nchi.
Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.
Kwa Mujibu wa mtandao wa Daily Monitor wa Uganda, umeeleza hatua hizo zilizoanza kuchukuliwa kuanzia jana Jumanne, Septemba 20, 2022 ikiwa ni saa chache baada ya vipimo vya maabara kuthibitisha mgonjwa wa kwanza aliyegundulika katika Wilaya ya Mubende iliyopo katikati ya nchi hiyo.
Meneja wa uhusiano wa umma wa Link Bus Services, mabasi ambayo hupita Magharibi kupitia Mubende, Tom Best Aliinde amesema ana wasiwasi kwamba wafanyakazi wao wanaotoa huduma kwa mamia ya wateja kila siku, wako hatarini.
"Tayari tumeweka hatua kadhaa za kujikinga kwa wafanyikazi wetu wote, abiria na umma kwa ujumla. Kama kawaida, tumejitolea kufanya kazi na Serikali na wadau wengine kudhibiti kuenea kwa Ebola,” amesema Aliinde.
Ebola ni ugonjwa wa virusi unaosambazwa hasa kwa kugusa maji au damu ya mtu aliyeambukizwa, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Hata hivyo, ugonjwa huo si rahisi kudhibitiwa, kwani unaweza kusambaa kwa kasi kupitia kugusa maji maji ya kutoka mwilini mwa muathiriwa.
Baadhi ya wasafirishaji waliohojiwa walisema wameamua kuchukua hatua za kujikinga wao wenyewe kwa kusafisha mabasi yao kwa JIK pamoja na kutoa maji na sabuni za kunawa kabla abiria yeyote hajaingia ndani ya basi.
Katika maeneo yote ya usafiri wa umma, ikiwa ni pamoja na kwenye vituo, hospitali, wamiliki wameanzisha utaratibu wa matumizi ya vitakasa mikono na glavu - hatua ambazo zilikuwa zimepungua baada ya kupungua kwa janga la Uviko19.
Katika Wilaya ya Kikuube, ambayo ipo karibu na Mubende ambapo washukiwa na waliothibitishwa wamesajiliwa, maofisa walifanya mkutano mkubwa kupanga njia za kuongeza ufuatiliaji na uhamasishaji wa jamii.
“Moja ya maazimio ya mkutano huo ilikuwa kuja na mpango wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. Pia tumeanza kuhamasisha jamii kufahamu kuhusu mlipuko wa Ebola,” amesema Ofisa wa habari wa Wilaya ya Kikuube, Faridah Ngabano, afisa wa habari wa Wilaya ya Kikuube.