MLIPUKO mkubwa umetokea na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wawili katika wilaya ya Nakaseke katikati mwa Uganda. Tukio hilo lilitokea katika mji mdogo wa Kapeeka, majira ya saa mbili kutoka Mji mkuu Kampala.
Walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa kifaa hicho kilikuwa kwenye rundo la vyuma chakavu, na mlipuko huo ulimuua mfanyabiashara wa vyuma chakavu aliyekuwa akipasha moto ili kuviyeyusha.
Polisi wamezingira eneo la tukio na kuanza uchunguzi kuhusu chanzo cha kilipuzi hicho. Msemaji wa polisi amesema kwamba wanaamini kuwa kifaa hicho kinaweza kuwa kilipuzi cha kale.
Nakaseke ni sehemu ya Pembetatu ya Luweero, ambako vita vilivyomuingiza Rais Yoweri Museveni madarakani miaka ya 1980 vilipiganwa. Na huko nyuma, mabaki ya vilipuzi yameua au kuwajeruhi watu katika eneo hilo.