Jeshi la ulinzi la taifa la Afrika Kusini (SANDF) Jumatatu limesema kwamba mkuu wake wa jeshi Lawrence Mbatha, alikuwa Moscow kwa mkutano wa pande mbili ambako atatembelea shule za kijeshi za Russia na kufanya mazungumzo na maafisa.
“Lazima ifahamike kwamba Afrika Kusini ina uhusiano wa kijeshi na mataifa mbalimbali barani humo na nje ya bara hilo,” ilisema taarifa ya SANDF na kuongeza kuwa mkutano huo nchini Russia ulipangwa mapema.
Mapema Jumatatu, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alisema msimamo wa nchi hiyo ni kutofungamana na upande wowote na hauipendelei Russia dhidi ya mataifa mengine na akasisitiza wito wake kwa suluhisho la amani kwa mzozo nchini Ukraine.
Ramaphosa alitoa maoni hayo katika jarida la kila wiki la rais. Wiki iliyopita, Marekani ilidai silaha zilipakiwa kwenye meli ya Russia, Lady R kutoka kambi ya jeshi la majini huko Cape Town mwishoni mwa mwaka jana, jambo ambalo lilizua mzozo wa kidiplomasia.