Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat, amelaani mapigano makali ambayo yamezuka nchini Chad kati ya polisi na waandamanaji katika mji mkuu.
"Ninalaani vikali maandamano ambayo yalisababisha vifo vya wanaume kadhaa huko #Tchad," mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika-AU, Bw Mahamat alisema.
"Ninatoa wito kwa wahusika kuheshimu maisha ya watu na mali na kupendelea njia za amani za kumaliza mizozo," aliendelea.
Watu wanaandamana kupinga serikali ya mpito ya kijeshi ya Chad na kutoa wito wa kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Polisi walitumia risasi na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji na baadhi ya maeneo ya N'Djamena yamezingirwa.
Mwandishi wa habari na polisi wameripotiwa kuuawa wakati wa maandamano hayo, lakini hakuna takwimu rasmi za majeruhi.
Wakati huo huo, msemaji wa Ufaransa alilaani matumizi ya silaha za mauaji dhidi ya waandamanaji na kukanusha kuhusika kwa Paris.