Mwanzilishi wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner, Yevgeny Prigozhin, ameiambia Afrique Media TV kwamba mamluki wake wataendelea kufanya kazi katika nchi za Afrika waliko.
"Tunaendelea kufanya kazi katika nchi zote tulikoanza au tunakofanya kazi hii ya ushirikiano na maendeleo kwa sasa," alisema katika mahojiano yaliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa pro-Kremlin TV.
"Iwapo usaidizi wa Kundi la Wagner unahitajika mahali popote ili kukabiliana na magenge na magaidi na kulinda maslahi ya watu wa nchi hizi, tuko tayari kuanza mara moja kutekeleza jukumu hili baada ya kukubaliana juu ya masharti."
Aliongeza kwamba "hakukuwa na hakutakuwa na kupungua kwa shughuli zetu barani Afrika".
Matamshi yake yalifuatia uvumi kuhusu uwezekano wa kuondolewa kwa mamluki wa Wagner kutoka Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Uvumi huo ulianza kuenea baada ya Bw Prigozhin kuandaa maasi ya muda mfupi nchini Urusi mnamo 24 Juni.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameshutumu mamluki wa Wagner kwa kujihusisha na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Mali na CAR.