Viongozi wa mataifa ya Afrika wanakutana mjini Addis Abbaba leo kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika unaofanyika chini ya kiwingu cha wimbi jipya la mapinduzi ya kijeshi barani humo na kujikongoja kwa juhudi za kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Pamoja na masuala hayo mawili mkutano huo pia unalenga kutafuta uungaji mkono wa kushinikiza bara la Afrika kupata uwakilishi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa yake kuelekea mkutano huo, shirika la kimataifa la masuala ya mizozo limesema suala la usitishaji mapigano nchini Ethiopia, kuunga mkono mazungumzo kwenye mzozo wa kanda ya Sahel na kuufanyia mageuzi ujumbe wa kijeshi nchini Somalia vinapaswa kuwa vipaumbele vya Umoja wa Afrika kwa mwaka huu.
Umoja wa Afrika ambao mwezi Julai utatimiza miaka 20 tangu kuundwa kwako umekuwa ukikosolewa kwa kushindwa kushughulikia mizozo inayozuka kila wakati ndani ya bara hilo la waakazi bilioni 1.3