Serikali ya Morocco imesisitiza kuwa mkutano mkuu wa mwaka wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia uliopangwa kufanyika Marrakesh kuanzia Oktoba 9 hadi 15 mwaka huu uko palepale licha ya jiji hilo kukumbwa na tetemeko la ardhi, Septemba 9 mwaka huu.
Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000 na kujeruhi huku likiacha wengine hawana makazi katika jiji hili ambalo ni kitovu cha utalii kwa nchi ya Morocco.
Gavana wa Benki Kuu ya Morocco, Abdellatif Jouahri amesema kuwa hali ya mambo imeanza kutengemaa katika jiji hilo na hakuna kizuizi chochote cha mkutano huo utakaojadili masuala ya fedha na uchumi kwa nchi wanachama 189.
"Wakati janga hilo limetokea, baadhi ya wakuu wa Benki ya Dunia na IMF walikuwa hapa. Wameona kilichotokea na wakafanya tathmini kisha wakatoa uamuzi kwamba mkutano utakuwa hapahapa kwa vile hakuna athari yoyote katika hoteli ambazo zitapokea wageni na eneo ambalo mkutano utafanyika.
"Tunategemea mkutano huu utakuwa wenye tija kwa Morocco na bara zima la Afrika katika kupaza sauti yetu kwa yale ambayo tunahitaji yafanyiwe kazi na taasisi hizo mbili kubwa," amesema Jouahri.
Ujenzi wa kijiji ambacho mkutano huo utafanyikia hapa Marrakesh unaendelea kwa kasi ambapo unategemewa kuwa na washiriki wapatao 3,500 wakiwa na mawaziri wa fedha, magavana wa benki kuu wa nchi wanachama pamoja na wadau watakaoambatana nao.
Lakini pia maeneo mengi ya Marrakesh, watu wamekuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida hasa utalii na biashara huku wageni wakiendelea pia kuingia.
Mkutano wa IMF na Benki ya Dunia, unafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika baada ya miaka 50 tangu ulipofanyika kwa mara ya mwisho mwaka 1973.