Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkutano SADC wabeba mambo 3 kwa Tanzania

Ce83e95373cdc523676668291a15dd4b Mkutano SADC wabeba mambo 3 kwa Tanzania

Sat, 13 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUTANO wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza ukibeba mambo kadhaa, matatu yakiigusa Tanzania moja kwa moja.

Mambo hayo matatu ni Kiswahili kuanza kutumika rasmi katika mikutano ya ngazi za kisekta za jumuiya hiyo, kutengenezwa na kuwekwa kwa sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi wa SADC katika Jengo la Amani katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia na maadhimisho ya miaka 40 ya SADC.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa mkutano huo unaofanyika kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Mawaziri wa SADC wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi alisema mkutano huo ni wa siku mbili na mambo hayo yatajadiliwa na kuamuliwa rasmi.

“Leo (jana) tunaanza kikao cha siku mbili cha Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC na katika mkutano huu wa siku mbili, mambo makubwa matatu yenye maslahi kwa Tanzania yatajadiliwa na kuamuliwa,” alisema Profesa Kabudi.

Akifafanua Profesa Kabudi alisema katika Kikao cha 39 cha Wakuu wa Nchi wa SADC Kiswahili kilipitishwa kuwa lugha ya nne ya SADC na kiliamuliwa kitumike katika mikutano ya baraza la mawaziri na mkutano wa wakuu wa nchi na sasa kitatumika pia katika ngazi ya kisekta.

“Sasa imeamuliwa si tu katika mikutano hiyo miwili bali katika mikutano yote ya kisekta. Kwa hiyo sasa Kiswahili kitatumika katika ngazi ya sekta ambayo ni hatua kubwa iliyofikiwa na ya kujivunia kwa nchi yetu. Sekta kama za afya, miundombinu, biashara, viwanda na nyingine zote, Kiswahili kitatumika,” alisema Profesa Kabudi.

Akizungumza kuhusu sanamu ya Mwalimu Nyerere, alisema kwa miaka takribani miwili, SADC iliamua kutengeneza sanamu maalumu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika Jengo la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere la Amani lililopo jijini Addis Ababa katika Makao Makuu ya AU.

“Mchakato unaendelea na tunaamini katika kikao hiki tunaamini tutakamilisha mchakato wa kumpata mtu atakayefua sanamu hiyo inayotakiwa iwekwe kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU),” alisema.

Alisema enzi za uhai wake, aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe alipendekeza na kueleza nafasi muhimu za Mwalimu Nyerere kama mwanzilishi wa AU mwaka 1963 na mwanaharakati wa ukombozi wa nchi za Afrika.

Profesa Kabudi alisema katika harakati hizo hasa za ukombozi wa nchi za kusini, makao makuu ya harakati yalikuwa Tanzania na Katibu Mkuu wa Kwanza wa Kamati ya Ukombozi wa Afrika alikuwa Mtanzania ambaye ni George Magombe na baadaye alikuwa Brigedia Jenerali Hashim Mbita.

“Mugabe na Museveni katika vikao vya AU walisema kama kuna kiongozi anayestahili heshima kwa ukombozi wa nchi za Afrika basi si mwingine bali ni Mwalimu Julius Nyerere. Hivyo Mugabe alipendekeza pawe na Jengo la Mwalimu Nyerere, ndio hilo la Amani,” alifafanua.

Alisema miaka miwili iliyopita SADC iliamua kumuenzi Nyerere kwa kutekeleza maoni ya Mugabe kutengeneza sanamu iwekwe katika jengo hilo kama kumbukumbu ya mchango wa Mwalimu Nyerere katika historia ya Afrika.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, jambo la tatu ni maadhimisho ya miaka 40 ya tangu SADC ilipoanzishwa kutoka Jukwaa la Kuratibu Harakati za Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCC) na kuwa SADC.

Alisema maadhimisho hayo yatafanyika sambamba na mada mbalimbali, vipindi vya televisheni na redio, midahalo na makongamano.

“Hii ina umuhimu mkubwa sana kwa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa viongozi waliosisi SADC, miongoni mwa viongozi wanane wa mwanzo ni Mwalimu Julius Nyerere katika mkutano uliofanyika mwaka 1979 Arusha na kuamua kuwa na SADC,” alisema Profesa Kabudi na kuongeza kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu.

“Tutakuwa tunasherehekea miaka 40 ya SADC Kiswahili kikiwa ni moja ya lugha rasmi za SADC, lakini pia tukiwa na sanamu maalumu ya kumuenzi na kumheshimu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa letu na muasisi wa SADC,” alisema.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri wa SADC, unahudhuriwa na mawaziri kutoka nchi zote 16 za jumuiya chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Veronica Dlhovo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz