Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkosoaji wa serikali ya Rwanda alikufa katika ajali - polisi

Mkosoaji Wa Serikali Ya Rwanda Alikufa Katika Ajali   Polisi Mkosoaji wa serikali ya Rwanda alikufa katika ajali - polisi

Fri, 20 Jan 2023 Chanzo: Bbc

Mwanahabari maarufu na mkosoaji wa serikali ya Rwanda alifariki katika ajali ya barabarani katika mji mkuu wa Kigali, polisi wameiambia familia yake.

John Williams Ntwali - ambaye alikuwa mhariri wa tovuti ya habari ya The Chronicles - alifariki Jumanne usiku wakati pikipiki aliyokuwa ameabiri ilipogongwa na gari eneo la Kimihurura, kaka yake Emmanuel Masabo aliambiwa na polisi.

Bw Masabo alisema alipigiwa simu na polisi Alhamisi mchana ili kuthibitisha utambulisho wa mwili huo katika chumba cha kuhifadhia maiti.

“Nilipofika walinipeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Niliona ni yeye na nikawathibitishia,” Bw Masabo aliambia BBC.

Aliongeza: "Hawakunipa maelezo zaidi... labda baadaye. Pia sikuwa na nguvu ya kuuliza zaidi [wakati huo]."

Tovuti ya habari ya Chronicles pia imethibitisha kifo cha mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 43 katika ujumbe wa Twitter. Alikuwa mhariri wa uchapishaji tangu 2021.

Bw Ntwali alikosoa serikali na chama tawala katika ripoti zake zilizoangazia ukosefu wa haki na masuala ya kijamii yanayowakabili Wanyarwanda kupitia chaneli yake ya YouTube, Pax TV-Ireme news.

Waungaji mkono wa serikali walimkosoa kuwa "mtu mwenye msimamo mkali" na kumshambulia mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii.

Waandishi wa habari na marafiki wameeleza kushtushwa na kifo chake.

Ameacha mke na binti.

Chanzo: Bbc