Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkosoaji mkuu wa Rais Kagame afa kifo chrnye utata

Anne Rwigara (23).jpeg Anne Rwigara.

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mashirika ya habari. Anne Rwigara, mdogo wa Diane Rwigara aliyejaribu kugombea urais nchini Rwanda dhidi ya Rais Paul Kagame mwaka 2017, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 41.

Anne, mmoja wa watoto wa mfanyabiashara maarufu wa zamani nchini Rwanda, Assinapol Rwigara, amefariki dunia siku ya Alhamisi nchini Marekani alikokuwa akiishi, kwa mujibu wa wanafamilia wake.

Mwanafamilia wa karibu aliliambia Shirika la Utagazaji la Uingereza (BBC) kwamba, Anne amefariki dunia nyumbani kwake California, nchini Marekani.

Mama yake Anne, Adeline Rwigara, anayeishi Kigali, aliiambia BBC kwa maandishi: “Yeye si mgonjwa. Ni suala la siku tu. Ni siri tu.”

Kwa mujibu wa taarifa, Anne alianza kusumbuliwa na maumivu ya tumbo kabla ya  umauti kumfika.

Baba yake, marehemu Assiponal, alifariki kwa ajali ya gari mwaka 2015. Familia ya marehemu ilidai kifo hicho kilipangwa, lakini hawakusema kilipangwa na nani.

Anne kulingana na wasifu wake alioutoa kortini mwaka 2017, anakumbukwa mwaka huo alipokaa gerezani na mama yake kwa siku kadhaa pamoja na dada yake, Diane Rwigara wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Ilikuwa baada ya uchaguzi wa urais wa 2017 ambapo dada yake mkubwa, Diane, alizuiwa kufanya kampeni kugombea kiti cha rais. Katika uchaguzi huo Rais Kagame alishinda kwa karibu asilimia 99 ya kura.

Mpaka sasa, hakuna maelezo yanayojulikana kuhusu chanzo cha kifo cha Anne Rwigara, aliyekuwa raia wa Marekani, kulingana na shirika la habari la Reuters.

Mama yake Anne, Adeline Rwigara, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kifo cha bintiye ni cha kutatanisha, kwani hakuwa mgonjwa.

Chanzo cha habari cha Sauti ya Amerika (VOA), miongoni mwa watu wa karibu wa familia ya Rwigara kinasema mtoto wa Rwigara alifariki nchini Marekani kutokana na kuugua ghafla.

Habari za kifo cha Anne zilianza kuenea kwenye mitandao ya kijamii Jumanne jioni.

Anne Rwigara pia amejitokeza mara kadhaa katika kesi ambazo familia yake imefungua kuhusiana na mali zao kikiwamo kiwanda cha tumbaku cha Premier Tabacco Company Ltd.

Sababu kuu ya kila kitu wakati huo ilikuwa kodi ya ambayo Serikali ilisema inaidai familia ya Rwigara.

Anne na mama yake walikaa gerezani kwa mwaka mmoja nchini Rwanda kwa tuhuma za kukwepa kulipa ushuru na makosa yaliyohusiana na uchaguzi nchini Rwanda.

Mikasa iliyopata familia

Licha ya kuwa familia ya kitajiri nchini humo, hawakuwahi kufurahia utajiri huo tangu baba yao, Assinapol Rwigara alipofariki kifo cha utata katika ajali mwaka 2015.

Mei 2017 dada yake Anne, Diane Rwigara, alitangaza kuwa atagombea katika uchaguzi wa Rais dhidi ya Rais Paul Kagame.

Lakini baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimzuia Diane kushiriki katika uchaguzi ulioshuhudia, Paul Kagame akiibuka na ushindi wa asilimia 98.8 kwa madai kuwa aliwasilisha majina ya watu waliokufa kama wadhamini wake wa kugombea kiti cha urais.

Agosti 30, 2017, nyumba ya Rwigara ilivamiwa, huku polisi wakisema alikuwa anachunguzwa kwa kughushi na kukwepa kulipa ushuru.

Familia ya Rwigara iliripoti kupotea kwa Diane, ikisema kwamba watu wasiojulikana waliokuwa na silaha wakiwa wamevalia kiraia walimkamata na kumshikilia kwa mtutu wa bunduki wakati nyumba ikipekuliwa, lakini polisi walikanusha wakidai alikuwa amekamatwa.

Septemba 2017 iliripotiwa kuwa, Diane bado hakuwa amepatikana na kwamba familia yake iliendelea kudai kuwa ametoweka.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa Diane alikuwa akituhumiwa kuhatarisha usalama na kughushi nyaraka.

Jeshi la polisi nchini humo liliandika katika mtandao wa Twitter (sasa X) kuwa wa Diane pamoja na familia yake walikamatwa baada ya kushindwa kuitikia wito wa polisi waliopewa siku kadhaa nyuma.

Diana na ndugu zake Anne Rwigara na mama yao, Adeline Rwigara, walituhumiwa kughushi nyaraka katika mchakato wa kutafuta wadhamini ili aweze kugombea urais katika uchaguzi uliomalizika miezi miwili iliyopita.

Akihojiwa na Kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, kabla ya kujitosa katika uchaguzi Diane alisema anajua kitakachompata lakini haogopi tena.

"Fisi akikukimbiza muda mrefu uoga huwa unapotea," alisema huku akikiri kuwa anaumizwa na hali ilivyo hasa ya watu kushindwa kuongea kwa uwazi kwa sababu ya hofu.

Kilichomtia matatani Diane ni kukumbushia uchunguzi wa kifo cha baba yake, Assinapol Rwigara, kilichotokea mwaka 2015.

Pamoja na ushupavu wake Diane hajawahi kufurahi siasa au utajiri wa baba yake ambaye alionekana kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya jeshi, siasa na biashara za nchi hiyo.

Diana ni mfanyabiashara na mwanaharakati wa haki za wanawake aliyezaliwa mwaka 1981, Rwanda na kitaaluma ni mhasibu.

Siku moja baada ya kutangaza nia yake ya kuwania Urais, mitandaoni zilionekana picha zikimwonyesha akiwa kama alivyozaliwa huku amejipumzisha juu ya kochi.

Diane anazikana picha hizo akisema si zake ingawa zilitengenezwa kwa umahiri wa hali ya juu ili kumdhalilisha na kumpunguzia nguvu kutimiza azma yake.

"Baada ya kuona picha hazikufua dafu, yakafuata mengine mengi ikiwamo kudaia kutumia majina ya watu, sikudanganya katika hili kama inavyoelezwa,” alisema Diana.

Juni 2018, Mamlaka ya Mapato ya Rwanda iliuza mashine za kiwanda cha tumbaku cha familia hiyo kwa zaidi ya Sh5 bilioni kwa nia ya kurejesha kile walichodai kuwa ni malimbikizo ya kodi ya zaidi ya Sh17 bilioni.

Mnada wa awali wa mali ya biashara ya familia ya Rwigara ya tumbaku iliyosindikwa ulipata zaidi ya Sh995 milioni.

Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International lilitoa wito kwa mahakama ya Rwanda kuhakikisha kwamba kesi hiyo haiwi njia nyingine ya kuwatesa wakosoaji wa serikali.

Oktoba 5, 2018, mahakama iliamuru kuachiwa huru kwa Diane na mama yake, Adeline kwa dhamana; hii ilikuja wiki chache baada ya kuachiwa mapema kwa wafungwa 2,140, ikiwa ni pamoja na Victoire Ingabire na Kizito Mihigo.

Hata hivyo, Diane na mama yake waliambiwa wasiondoke katika mji mkuu, Kigali, bila kibali, na kesi yao ingeendelea.

Maseneta kadhaa wa Marekani, wakiwemo Dick Durbin, Ann Wagner, Patrick Leahy na Barbara Lee, pamoja na wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu ya Bunge la Marekani walitoa wito kwa serikali ya Rwanda kufuta mashtaka hayo.

Hata hivyo, maofisa wa Rwanda waliwashutumu wanasiasa wa Marekani kwa kuingilia taratibu zao za mahakama.

Hawako peke yao

Licha ya Rwanda kutajwa kuongoza duniani kwa kuwa na wabunge wanawake zaidi ya asilimia 61, mateso huwakuta wale wanaoipinga Serikali.

Mwaka 2003, Alvera Mukabaramba alijaribu kugombea urais lakini alijitoa na kuungana na Rais Kagame.

Mwaka 2010, Victorie Ingabire aliyekuwa akiishi Uholanzi alikwenda Rwanda kugombea urais, lakini aliingia matatizo baada ya kuzungumzia mauaji ya Kimbari na kudai kuwa aliyakana hivyo alihukumiwa kifungo cha miaka 15.

Leon Orsmond, mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Afrika Kusini, ambaye alimsaidia Diane katika kampeni yake ya mitandao ya kijamii pia alipotea nchini Rwanda tangu Februari 2018.

Kabla ya kutoweka, Orsmond hakuficha chuki yake kwa serikali ya Kagame.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live