Theresa Kufuor, Mke wa Rais wa zamani wa Ghana, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87.
"Ukarimu wake, fadhili na neema vilikuwa vya kipekee," alisema rais wa sasa wa nchi katika tangazo siku ya Jumatatu.
Bi Kufuor alihudumu kama Mke wa Rais kuanzia Januari 2001 hadi Januari 2009 na anakumbukwa kwa kazi yake ya kujitolea katika kuendeleza huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini Ghana.
Juhudi zake za utetezi zilikuwa muhimu katika kuanzishwa kwa sera inayotoa huduma ya bure ya uzazi, ambayo ilipunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya vifo vya uzazi na watoto nchini.
Mnamo 2007, alitetea mageuzi ya sera kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa Unesco wa Elimu ya Msingi ya Lazima kwa Wote (FCUBE) kwa watoto wa umri wa mdogo.
Alizaliwa kama Theresa Mensah tarehe 25 Oktoba 1935 huko Kumasi, Ghana, aliendelea kuwa na kazi ya kuridhisha kama mkunga na akapata pongezi kutoka kwa Waghana kwa kudumisha hadhi ya kawaida katika miaka yake minane katika maisha ya umma kama mke wa rais.
Aliolewa na Rais wa Zamani John Agyekum Kufuor mnamo 1962 baada ya kukutana kwenye densi ya maadhimisho ya Siku ya Jamhuri huko London mwaka mmoja kabla. Theresa Kufuor ameacha mumewe na watoto wao watano.