Makumi ya maofisa wa polisi wenye silaha nzito jana Jumatano Mei 3, 2023 walivamia makazi ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu na kukamata magari ambayo walisema yalidaiwa kuibwa na mke wa Rais huyo wa zamani.
Polisi walisema wameanzisha uchunguzi kufuatia ripoti ya wizi wa magari matatu na kufanikiwa kupata mali hiyo katika makazi ya mke huyo (Esther) wa Lungu katika kitongoji kimoja kilichopo katika mji mkuu wa Lusaka.
“Mtuhumiwa ameitwa kufika kituo cha polisi leo,” msemaji wa jeshi la polisi, Danny Mwale alisema.
Polisi walisema mke wa Lungu anadaiwa kupora magari hayo, lori aina ya Mitsubishi na magari mawili madogo aina ya Toyota Sedan, kutoka kwa mwanamke mmoja Agosti 2022.
Mwathirika, ambaye ametajwa lakini hajaelezewa zaidi, alilazimishwa kusalimisha magari hayo baada ya kuendeshwa hadi kwenye makazi ya mke huyo wa Rais wa zamani, polisi walisema.
Wafuasi wengi wa Lungu hasa kutoka chama kilichowahi kutawala cha Patriotic Front, walifika kwenye nyumba hiyo kuonyesha mshikamano kwa Lungu na familia yake, mwandishi wa AFP alishuhudia.
Awali, polisi walionekana wakipekua magari yaliyokuwa yameegeshwa ndani ya uzio wa Lungu.
Mwaka 2021, Lungu alishindwa kwenye uchaguzi mkuu dhidi ya Rais Hakainde Hichilema, ambaye kabla ya kushinda uchaguzi huo kwa kishindo, alikuwa kiongozi mkongwe wa upinzani.
Raphael Nakachinda, msemaji wa chama cha Lungu, aliishutumu Serikali ya Hichilema kwa kutoa vitisho na kutaka kulipiza kisasi.