Mke aliye na umri wa miaka 53 ameshtakiwa kwa kuchoma uso wa mumewe na kemikali ya betri, asid.
Ann Njambi, ambaye ni mfanyabiashara alishtakiwa kwa kumwumiza mumewe Antony Mwangi kwa kumchoma kwa asid mnamo Aprili 1, 2023.
Njambi alikana alimsababishia mumewe majeraha katika mtaa wa Balonzi ulioko Muthaiga Kaskazini.
Akiomba aachiliwe kwa dhamana, Njambi alimweleza hakimu mkazi Monica Kivuti kwamba kisa hicho kilitokana na makabiliano na mumewe akimwitisha pesa.
“Tulivurugana na mume wangu nikimwitisha pesa za gari langu aliyoiuza,” Njambi alisema.
Mbali na kuchomwa uso mlalamishi (Mwangi) alichapwa masumbi na mshtakiwa alipomkabili akitoka kuoga asubuhi ya siku ya kisanga, Aprili 1, 2023.
Upande wa mashtaka umesema mahojiano yamebaini mshtakiwa na mumewe wamekuwa wakilumbana kwa muda tangu 2017.
Upande wa mashtaka haukupinga mshtakiwa akiwachiliwa kwa dhamana. Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Ksh15, 000. Kesi hiyo imeorodheshwa kusikizwa Septemba 14, 2023.