Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Abdoulaye Bathily, amesisitizia haja ya mshikamano na kuratibiwa hatua kitaifa ili kukabiliana na mgogoro ulioikumbwa Libya hivi sasa, kufuatia mafuriko mabaya yaliyoyakumba maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, mapema mwezi huu.
Ameyasema hayo mjini Benghazi, wakati alipoonana na Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa jeshi la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo, na wamejadiliana pia juhudi za misaada ya kibinadamu zinazoendelea katika maeneo yaliyokumbwa na maafa.
Bathily ameandika katika mtandao wa kijamii wa X yaani Twitter ya zamani baada ya mazungumzo hayo kwamba: "Nimerejea mwito wangu kwa wadau wote kuendeleza mshikamano wa aina yake unaooneshwa hivi sasa na Walibya wote katika nyakati hizi ngumu na kuongeza juhudi kuelekea kuitishwa uchaguzi na kuunganishwa taasisi za taifa ili kushughulikia vyema changamoto za siku za usoni. Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Abdoulaye Bathily
Vilevile ameandika: "Nimesisitizia tena ulazima wa kuruhusiwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kuwafikia waathiriwa wote wa mafuriko hayo na hasa wale wanaoishia kwenye maeneo yaliyoharibiwa zaidi na mafuriko.
Tarehe 10 mwezi huu wa Septemba, kimbunga cha Daniel kilipiga maeneo ya mashariki mwa Libya na kusababisha mafuriko makubwa na mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita. Maelfu ya watu wamepoteza maisha na makumi ya maelfu wamehama makazi yao, huku miundombinu ya maeneo yalo yakiharibiwa vibaya.
Libya imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu alipopinduliwa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi mwaka 2011. Kuna serikali mbili hasimu zinatawala nchi hiiyo hivi sasa. Mgogoro huo wa kisiasa umekuwa na athari mbaya kwa nchi, kwa uchumi, miundombinu iliyoharibiwa, na mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao.