Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameeleza wasiwasi wake juu ya kukamatwa kwa waangalizi wa Uchaguzi huko Zimbabwe huku pia kukiwa na vitisho kwa wapiga kura, vurugu na unyanyaswaji.
Guterres amewataka viongozi wa siasa na wafuasi wao kukataa kila aina ya vurugu na kuheshimu haki za binadamu na sheria.
Katibu Mkuu huyo amewataka wanasiasa kumaliza tofauti zao kwa amani na kwa kutumia njia za kitaasisi na kisheria, vilevile amezihimiza mamlaka husika kutatua migogogoro kwa uwazi, haki na njia za haraka.
Tume ya uchaguzi imetangaza kuwa Rais Emmerson Mnangwagwa ameshinda katika uchaguzi huo kwa asilimia 52.6 ya kura.
Hata hivyo upande wa upinzani nao umedai kushinda uchaguzi huo, kutokana na kile walichokiita "wizi mkubwa wa kura na kutokuwepo kwa demokrasia".
Wiki iliyopita zaidi ya waangalizi 40 wa kura walikamatwa wakati wakijaribu kukusanya hesabu zao za kura ili kulinganisha na hesabu rasmi.