Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi ameahidi kuiunga mkono Somalia katika mvutano wake na Ethiopia juu ya mkataba wa bandari na Somaliland.
Jumatatu, Ethiopia ilisaini mkataba wa mpango wa kutumia bandari moja na Somaliland, uamuzi ambao ulizua ukosoaji mkubwa kutoka Somalia.
Somalia, ambayo inaichukulia Somaliland kuwa sehemu ya ardhi yake, imelaani mpango huo, na kutaja kuwa ni kitendo cha "uchokozi" na ukiukaji wa uhuru wake.
Katika mazungumzo ya simu na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Rais al-Sisi aliahidi "msimamo thabiti wa Misri kuiunga mkono Somalia pamoja na kuimarisha ulinzi na utulivu," msemaji wa al-Sisi, Ahmed Famy alisema siku ya Jumanne, akiongeza kwamba viongozi hao wawili pia walijadili kuhusu "maendeleo ya kikanda" na uhusiano wa nchi mbili.
Rais Mohamud pia alizungumza kwa njia ya simu na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad kuhusu uhusiano wa pande mbili wa kikanda wenye maslahi ya pande zote, ofisi ya rais wa Somalia ilisema.
Umoja wa Ulaya umekosoa mpango huo, ukitaka kuheshimiwa kwa "umoja, mamlaka na uadilifu wa ardhi" ya Somalia.