Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza kuwa nchi hiyo haijafunga kivuko cha Rafah, lakini utawala wa Kizayuni wa Israel unazuia misaada kuingia Gaza.
Ahmed Abu Zeid, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri amesisitiza kuwa, kivuko cha Rafah kiko wazi tangu mwanzo wa mgogoro wa Ukanda wa Gaza na hakijafungwa katika hatua yoyote ile, lakini utawala wa Kizayuni wa Israel unazuia misaada kuingia Gaza kupitia njia mbalimbali.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri amepinga vikali madai kwamba nchi hiyo inakataa na haitaki kuafikiana na kuunga mkono haki za Wapalestina na kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Wakati huo Rafiq Abdes Salam, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Tunisia amekosoa misimamo ya Cairo kuhusiana na matukio ya Gaza na sera serikali ya Misri ya kufuata siasa za Marekani kuhusiana na jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza na kusema kuwa Gaza inayozingirwa na utawala wa Kizayuni wa Israel inapambana kwa niaba ya Ulimwengu wote wa Kiarabu.
Hapo awali, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ilikuwa imetoa taarifa ikilaani kufungwa kivuko cha Rafah katika mpaka wa Misri na Ukanda wa Gaza na kutangaza kwamba, katika kkipindi cha miaka 17 ya mzingiro wa kikatili, karibu lori 500 za mizigo zilikuwa zikiingia Gaza kila siku, na sasa kupunguzwa kwa malori hayo hadi lori 20 kwa siku ni njama ya Kimarekani-Kizayuni ya kujaribu kuhadaa walimwengu na kuvuruga mawazo ya umma kwamba mgogoro mbaya wa Gaza umetatuliwa.
Kivuko cha Rafah kinahesabiwa kuwa ndicho kiunganishi pekee kati ya Gaza na ulimwengu wa nje, na tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya wakazi wa Gaza utawala huo wa Kizayuni umekuwa ukitishia kukishambulia kivuko hicho iwapo msaada wowote utaingizwa Gaza.
Israel imekilipua kivuko hicho mara kadhaa kwa mabomu, lakini Misri ilitangaza kwamba inakijenga upya.