Hali ya afya inayoendelea kudorora nchini Sudan, huku kukiwa na ongezeko la magonjwa ya milipuko ya msimu, imeibua wasiwasi mkubwa wakati huu pia kukiendelea mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa RSF.
Wizara ya afya nchini Sudan, imekiri kuibuka kwa visa vya homa ya dengue, malaria, na kipindupindu katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Katika taarifa yake iliyochapishwa Jumanne, wizara hiyo imeripoti vifo 21 vinavyohusishwa na kipindipindu katika majimbo ya Khartoum na Gedaref.
Shirika la habari la kibinafsi la Sudan Tribune, siku ya Jumatano liliripoti kuwa matukio ya homa ya Dengue yameongezeka hadi takriban 700, likimnukuu kaimu waziri wa afya Haitham Ibrahim.
Kaimu waziri huyo alisema mlipuko wa homa ya Dengue umesambaa katika majimbo nane kukiwemo Red Sea, Kassala, Gedaref, Gezira, Sinnar, Kordofan Kaskazini na Kusini na pia Darfur Kaskazini, waziri huyo akihusisha kuenea kwa ugonjwa huo na kuongezeka kwa mbu kuzaana wakati wa mvua zinazoendelea kunyesha.
Katika jimbo la Gedaref, kampeni imeanzishwa ya kukabiliana na mlipuko huu kwa ushirikiano wa WHO, Unicef na timu ya usaidizi.