Kuna uwezekano mkubwa kwamba wasaidizi wa mhubiri ‘tata’ Paul Mackenzie, bado wapo katika msitu mkubwa wa Shakahola uliopo pwani ya kusini mwa Kenya, hii inatokana na zoezi la ufukuaji makaburi kugundua miili iliyozikwa hivi karibuni.
Mtandao wa Nation umeripoti kuwa vyanzo vya karibu vinavyohusika katika zoezi la ufukuaji, vimefichua kwa kujiamini kwamba, huenda miili hiyo imezikwa mwezi mmoja uliopita wakati timu inayohusika na zoezi hilo, ilipochukua mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuanza tena ufukuaji wiki iliyopita.
"Makaburi hayakuwa na kina kirefu, na yalikuwa na udongo uliolegea juu na majivu pembezoni, mengine yalionekana kuwa yamechimbwa upya," kimesema chanzo hicho.
Hii inaibua swali la kama kunaweza kuwa na watu msituni ambao bado wanafanya maziko ya wafuasi wa Mackenzie, miezi mitatu baada ya kuwa amekamatwa.
Afisa wa upelelezi aliye karibu na uchunguzi amethibitisha kuwa watu zaidi wanaoaminika kuwa ni washirika wa karibu Mackenzie, wanaaminika kujificha katika msitu huo.
“Tunawafuatilia, tunadhani ni wale waliojificha msituni wakati wa zoezi la kuwasaka na kuwaokoa, lakini hatukata tamaa hadi tuwapate, Jumatatu walituma ujumbe kupitia kwa wafugaji wakiwaambiwa watuonye tusiendelee na operesheni hiyo,” kimedokeza chanzo hicho.