Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miili ya watu waliovalia sare za kijeshi yaripotiwa katika mitaa ya Sudan

Miili Ya Watu Waliovalia Sare Za Kijeshi Yaripotiwa Katika Mitaa Ya Sudan Miili ya watu waliovalia sare za kijeshi yaripotiwa katika mitaa ya Sudan

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Bbc

Mapigano makali yanaripotiwa kuendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na katika eneo la magharibi la Darfur, ambako mamia wanasemekana kuuawa katika mapigano hayo yanayoendelea.

Walioshuhudia wameliambia shirika la habari la AFP kwamba miili ilitapakaa katika mitaa ya mji wa Omdurman siku ya Alhamisi katika ongezeko la hivi punde la ghasia kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

"Miili ya watu waliovalia sare za kijeshi imetanda katika mitaa ya katikati mwa jiji baada ya mapigano hapo jana," shahidi alinukuliwa akisema.

Magharibi mwa nchi hiyo, takriban watu 700 wameripotiwa kuuawa katika mapigano ya Darfur Magharibi, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Zaidi ya wengine 300 wameripotiwa kutoweka kufuatia mapigano huko El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, taarifa hiyo iliongeza.

Mashahidi wameishutumu RSF kwa kuwalenga na kuwaua watu wasio Waarabu katika mapigano hayo.

Ubalozi wa Marekani mjini Khartoum ulisema "umesikitishwa sana na ripoti za mashahidi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na RSF na wanamgambo washirika".

Lakini RSF inasema haihusiki katika kile inachoelezea kama "mgogoro wa kikabila".

Maelfu ya watu wamevuka hadi Chad katika siku chache zilizopita wakikimbia moto huo.

Takriban watu milioni sita wamelazimika kutoka makwao tangu vita vilipoanza katikati ya mwezi wa Aprili.

Chanzo: Bbc