Miili ya maafisa watatu wa kijeshi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu - waliouawa katika shambulizi la wanamgambo nchini Somalia - imewasili Abu Dhabi.
Taarifa ilisema afisa wa nne ambaye alipata majeraha wakati wa shambulio la Jumamosi alifariki alipowasili UAE.
Maafisa wa Imarati walisema maafisa hao wa kijeshi wamekuwa Somalia wakiwafunza wanajeshi wa eneo hilo.
Mwanajeshi wa Bahrain pia aliuawa katika shambulio hilo, ambalo kundi la Kiislamu la al-Shabab linasema lilitekeleza.
Katika taarifa yake ya kuomboleza mauaji ya mwanajeshi wake, jeshi la Bahrain limelaani shambulio hilo na kulitaja kuwa ni "kitendo cha uchokozi".
Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba anayedaiwa kuwa mshambulizi, mwanajeshi wa Kisomali ambaye alikuwa akikaa katika kambi hiyo, hivi karibuni alijitenga na al-Shabab.
Shambulio hilo lililenga wanajeshi katika Kambi ya Kijeshi ya Jenerali Gordon katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alilaani shambulizi hilo na kuamuru vikosi vya usalama vya nchi hiyo kufanya "uchunguzi wa kina na wa haraka".
Al-Shabab inaendelea kufanya mashambulizi ya kuua nchini Somalia licha ya mashambulizi makali ya kijeshi dhidi ya kundi hilo yaliyofanywa na wanajeshi waserikali kuu tangu Agosti 2022.