Thomas Tumusifu Buregeya anatamani angalikuwa anasoma kwa ajili ya mitihani yake ya mwisho ya shule, limesema shirika la habari la Reuters.
Badala yake, anatafuta riziki ya kufanya kazi zisizo za kawaida katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya wimbi la ghasia za waasi kuvuruga maisha yake tena.
Buregeya alikimbia mji wa Kibumba na familia yake mwezi Oktoba huku kukiwa na mashambulizi mapya ya kundi la waasi la M23 - mara ya tatu katika kipindi cha miaka 15 amelazimika kutoroka nyumbani kwake na hajaweza kusoma kwa mwaka mzima. Sasa ana umri wa miaka 22 na bado anasubiri kumaliza shule.
Buregeya alitoroka mji wa Kibumba na familia yake mwezi Oktoba huku kukiwa na mashambulizi mapya ya kundi la waasi la M23 - mara ya tatu katika kipindi cha miaka 15 akilazimika kutoroka nyumbani kwake na hajaweza kusoma kwa mwaka mzima.
Sasa ana umri wa miaka 22 na bado anasubiri kumaliza shule.
“Nikiwa katika kambi hii naona...walio katika mwaka wa mwisho wa masomo kama mimi, inaniuma sana, najiuliza ni lini nitamaliza masomo, miaka inasonga,” alisema.
Yeye ni mmoja wa vijana 750,000 wa Congo ambao masomo yao kwa sasa yamekatizwa kutokana na ukosefu wa usalama katika majimbo ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Ituri, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) lilikadiriwa idadi hiyo mwishoni mwa mwezi Machi.
Katika kambi ndogo iliyo karibu na kanisa la kiinjili nje ya mji mkuu wa mkoa wa Goma, Buregeya anatumia muda wake kuegemea ukuta wa bati wa kanisa au kucheza karata na marafiki wa shule pia waliofurushwa kutoka eneo la Kibumba, kulingana na Reuters.
Tangu Januari 2022, shule zipatazo 2,100 mashariki mwa Congo zimelazimika kufungwa kwa sababu ya mapigano ya kivita, kulingana na UNICEF.
Uharibifu unaweza kuwa wa muda mrefu. Bila kupata elimu, watoto na vijana wanaweza kukosa nafasi ya kukuza ujuzi unaohitajika ili kuondokana na umaskini na kuondokana na changamoto za kiuchumi ambazo zinasaidia kuchochea migogoro katika maeneo kama vile Mashariki ya Congo yenye madini, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2011 kuhusu elimu ya kimataifa na migogoro inayohusisha silaha.