Idara ya afya nchini Afrika Kusini imeanzisha uchunguzi kuhusu kauli iliyotolewa na waziri wa afya wa mkoa huo kwa mgonjwa wa Zimbabwe aliyekuwa akipatiwa matibabu.
Katika kanda ya video iliyovuma sana mtandaoni, Dkt Phophi Ramathuba anaonekana akimkemea mgonjwa wa Zimbabwe ambaye hakuwa na vibali vya kufanyiwa upasuaji katika hospitali moja katika mkoa wa Limpopo nchini Afrika Kusini.
Maoni yake yamelenga kuwalaumu raia wa kigeni kwa kuchangia mfumo mbaya wa afya nchini.
Dk Ramathuba alimwambia mgonjwa kwamba Zimbabwe inapaswa kuwajibika kwa masuala yake ya afya na si Afrika Kusini.
Aliongeza kuwa Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa hakuchangia bajeti ya afya ya Afrika Kusini.
Vyama vya upinzani vinadai kujiuzulu kwa afisa huyo na vilisema anapaswa kukemewa kwa kumdhalilisha mgonjwa.
Hata hivyo, Dk Ramathuba amesema anasimama na maoni yake, akiongeza kuwa jimbo la Limpopo, ambalo liko mpakani na Zimbabwe, lina "mmiminiko wa raia wa kigeni ambao wanazonga mfumo wa afya wa mkoa huo na kusababisha madaktari kufanya kazi chini ya shinikizo".
Pia alisema maoni yake hayapaswi kueleweka vibaya kama chuki dhidi ya wageni.
Mgonjwa huyo, alisema, alimwambia kwamba alihusika katika ajali ya barabarani katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, na alishauriwa kuvuka mpaka kutafuta matibabu.