Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgomo madereva wa malori Kenya waathiri biashara

Malori Kenya Mgomo madereva wa malori Kenya waathiri biashara

Wed, 5 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Biashara kwenye mpaka wa Kenya na Uganda imeathiriwa baada ya madereva wa malori kutoka Kenya kugoma kwa kupinga kufanyiwa vipimo vya Covid-19 kwa lazima.

Vipimo hivyo vinavyogharimu dola 30 ni sawa na shilingi 3,394 za Kenya na madereva wanahitaji kupimwa kila baada ya siku 14. Vipimo hivyo ni vya lazima licha ya madereva hao kuonyesha nyaraka za kuwa wameshapimwa na hawana virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, wanapotaka kuingia nchini Uganda.

Madereva hao wanadai kuwa vipimo hivyo ni njama za mamlaka ya Uganda za kuwatwalia fedha zao. Sasa, wameapa kutorejea kazini hadi mwafaka baina ya serikali za mataifa hayo upatikane. Mgomo huo unaingia siku ya nne leo Jumanne.

Mgomo huu unajiri chini ya mwaka mmoja baada ya mwingine kama huo kutokea mwaka uliopita ambapo maafisa wakuu wa mataifa hayo kuafikiana kuondoa vikwazo hivyo. Mgomo huo ulisababisha urefu wa kilomita 50 wa malori 4,500 yaliyounda msongamano upande wa Kenya kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Iwapo mgomo huu hautasitishwa, huenda taswira kama hiyo ikashuhudiwa tena. Mamia ya madereva hao sasa wamekwama katika mpaka wa Busia-Malaba huku bidhaa ambazo zilikuwa zisafirishwe nchini Uganda zikihofiwa kuharibika.

Madereva hao sasa wanazitaka serikali za mataifa husika kuingilia kati na kuangazia kilio chao. Msongamano huo huenda pia ukachangia kuongezeka kwa visa vya virusi vipya vya Omicron kwa mujibu wa wataalamu wa matibabu, iwapo hatua za dharura za kutafuta suluhisho hazitapatikana kwa dharura.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, Uganda iliagiza bidhaa zenye kima cha dola milioni 674 nchini Kenya mwaka 2020. Mamlaka za mataifa ya Kenya na Uganda hazijatoa tamko lao kuhusu mgomo huo unaoendelea kuchafua sio tu mazingira ya biashara lakini pia mahusiano ya mataifa hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live