Waziri mkuu wa zamani wa Sudan ameonya kuwa mzozo nchini mwake unaweza kuwa mbaya zaidi kuliko wa Syria na Libya.
Abdalla Hamdok alisema mapigano hayo yatakuwa "jinamizi kwa ulimwengu" iwapo yataendelea.
Jeshi la Sudan linasema kuwa linashambulia mji mkuu Khartoum kutoka pande zote, kwa kutumia silaha nzito nzito.
Mapigano ya takriban wiki mbili yamesababisha vifo vya mamia, huku makumi ya maelfu ya watu wakiikimbia nchi.
Kuongezwa Alhamisi usiku wa muda wa usitishaji vita kati ya pande zinazohasimiana ulifuatia juhudi kubwa za kidiplomasia za nchi jirani, pamoja na Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa.
Lakini nyongeza ya saa 72 haijafanyika.Mashambulio ya anga, vifaru na mizinga yanaripotiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo ya Khartoum.