Mfumo wa elimu nchini Afrika Kusini umeshindwa kuwasaidia watoto maskini sana kwa mujibu wa wazazi, waalimu na vijana wenyewe.
Watoto wengi nchini Afrika Kusini wamelazimika kutumia saa nyingi kutembea kutoka na kwenda shule kila siku, mara nyingi katika mazingira hatarishi. Inadaiwa kuwa wamechoka sana, na hawawezi kutimiza uwezo wao wa kielimu.
Asubuhi katikati ya wiki katika kaya ya Nhlangothi katika kijiji kidogo huko Starford KwaZulu-Natal ni muda wa harakati nyingi kwa ndugu watano ambao wanajitayarisha kwenda shule.
Luyanda Hlali, anachukua kuni ambazo ziliwekwa usiku uliopita, anazichanganya na mavi ya ng’ombe na kuanza kuwasha moto kwa ajili ya kuchemsha maji katika kijumba kidogo cha matope.
Hawezi kulala kwa muda mrefu, anatakiwa kufanya kazi za nyumbani na kujitayarisha kwenda shule – ambayo iko katika mji wa uchimbaji makaa wa Dundee, kilometa 10 kutoka kijijini kwake.
Wakati wa majira ya baridi, anakumbana na giza, baridi kali na safari hatari kwa msichana mdogo ambaye anatembea kupitia kwenye msitu kabla ya kuweza kuipata barabara.
“Naamka na kuianza siku yangu nyakati za saa kumi na nusu alfajiri nakwenda kuchukua kuni na kuwasha moto, halafu naoga na kuvaa nguo na kuondoka kiasi cha kama baada ya saa 11 hivi.” Luyanda Hlali ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tisa ambaye anatembea kwenda shule.
“Kwa kawaida nafika shule nyakati ya saa moja asubuhi na nikiwasili nakuwa nimechoka. Mara nyingi najitahdi kuwa makini katika kile ambacho mwalimu anakisema na mara nyingine najikuta nimesinzia. Waaalmu wanaponiita, ninachoweza kuwaeleza ni kwamba nimechoka.”aliongeza mwanafunzi huyo