Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amemteua Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake, na kumfanya mwanasiasa huyo mkongwe kuwa mwanamke wa kwanza kuwania urais kwa tiketi ya chama kikuu cha siasa.
Bi Karua, aliyekuwa waziri wa sheria na mgombeaji urais, anatoka eneo la kati ambalo lina idadi kubwa zaidi ya wapiga kura waliosajiliwa nchini.
Iwapo atachaguliwa mwezi Agosti mwanasiasa huyo mkongwe atakuwa naibu wa rais wa kwanza mwanamke wa Kenya.
Lakini Martha Karua ni nani?
Martha Karua alizaliwa tarehe 22 mwezi Septemba 1957 na ni mama wa watoto wawili.
Alianza shule katika shule ya msingi ya Mugumo Primary na baadaye kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Kabare Girls katika eneo la Kerugoya. Katika masomo yake ya O level, mara ya kwanza alijiunga na shule ya upili ya Kiburia baadaye akaelekea Ngiriambu Girls Secondary na hatimaye shule ya upili ya Karoti girls ambapo alikalia mtihani wake wa cheti cha Afrika mashariki.
Baadaye alijiunga na shule ya upili ya Nairobi Girls kwa msomo ya A level. Alihitimu na shahada ya sheria kutoka chuo kikuu cha Nairobi 1980, kabla ya kujipatia Diploma katika mafunzo ya sheria 1981.
Kazi ya kuwa mwansheria: Alihudumu kuwa hakimu katika mahakama kadhaa miaka ya 1980 hadi 1987, ambapo alianza kuhudumu kama wakili hadi 2002. Bi Karua alikuwa na jukumu muhimu katika upanuzi wa demokrasia ncini Kenya na masuala ya Jinsia wakat wa harakati za kupigania vyama vingi miaka ya tisini.
Alikuwa miongoni mwa mawakili waliojipatia jina la 'Young Turks' ambao waliipinga serikali ya aliyekuwa rais wa Kenya Daniel Arap Moi na kufanikiwa kuleta siasa za vyama vingi nchini Kenya.
Akiwa Wakili , aliwawakilisha wapiganiaji wa haki za kibinadamu pamoja na wanaharakati wa kisiasa waliokosana na utawala wa rais Moi. Baadhi ya kesi alizowakilisha ni pamoja na ile ya uhaini dhidi ya bwana Koigi Wamwere na marehemu Mirugi Kariuki mwaka wa 1990.
Siasa: Alichaguliwa mara ya kwanza kama mbunge wa Gichugu 1992 na kuhudumu hadi 2013 wakati alipowania urais na kumaliza wa sita akiwa na kura 43,881.
Bi Karua amehudumu kama waziri ;katika wizara ya maji , na ile ya haki hadi alipojiuzulu kwa ghafla baada ya kukosana na aliyekuwa rais Mwai Kibaki mwaka 2008.
Alikuwa akijulikana kwa jina la utani 'Iron Lady' likimaanisha mwanamke mkakamavu na asiyetingisika kutokana na umaarufu wake katika jukumu la kutetea serikali yake.
Katika Uchaguzi wa 2017, aliwania kiti cha ugavana cha Kirinyaga lakini akapoteza kwa Anne Waiguru . Alikwenda mahakamani kupinga matokeo hayo akidai udanganyifu , lakini akapoteza tena katika mahakama kuu, mahakama ya rufaa na mahakama ya kilele. Alichukua suala hilo hadi katika mahakama ya haki ya Arusha , ambapo aliishtaki serikali ya Kenya kwa kumnyima uhuru wa kupata haki yake .
Katika kesi yake aliwasilisha ushahidi wa kanda ya video aliowasilisha mbele ya mahakama kuu , lakini uliibwa na kupotea ulipokuwa chini ya usimamizi wa mahakama hiyo, lakini ikatoa uamuzi bila ya kufanya uchunguzi. Mahakama hiyo iliipata serikali ya Kenya na makosa na ikamzawadi ksh2.7 million kwa kukiuka uhuru wake wa kupata haki.