Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfahamu Engola Waziri aliyekatishwa uhai na mlinzi wake

Waziri Kazi Risasi Mfahamu Engola Waziri aliyekatishwa uhai na mlinzi wake

Tue, 2 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Charles Okello Macodwogo Engola alizaliwa Oktoba 12, 1958, wazazi wake wakiwa ni Chifu Nasan Engola na mama yake ni Ketula Engola kutoka Awangi Wilaya ya Oyam Kaskazini mwa Uganda.

Kulingana na wasifu wake katika tovuti ya Bunge la Uganda, alipata Astashahada (Diploma) kutoka Shule ya Soroti, katika Jiji la Soroti, iliyopo Mashariki mwa Uganda.

Shahada yake ya kwanza ya Masomo ya Maendeleo, alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), mwaka 2010. Shahada yake ya pili, ambayo ni ya Uzamili ya Utawala na Usimamizi wa Umma pia aliipata kutoka KIU, mwaka 2013.

Kuhusu kujiunga na Jeshi

Alijiunga na Jeshi la Uganda na akiwa huko aliweza kuwa Kamanda wa UPDF 501 Brigade, yenye makao yake makuu Opit, katika Wilaya ya Gulu, na baadaye alipandishwa cheo hadi kuwa Kanali. Alistaafu jeshini 2007.

Kuhusu Siasa

Wakati wa uchaguzi wa kitaifa wa 2006, Engola aliwania nafasi ya Uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Oyam kwa tiketi ya chama tawala cha NRM.

Engola alishinda kwa kishindo cha asilimia 93 ya kura. Alichaguliwa tena mwaka 2011 na alihudumu kama Mwenyekiti wa wilaya ya Oyam kwa muda wa miaka 10 mfululizo, kuanzia 2006.

Mnamo 2016 alishinda kiti cha ubunge cha Oyam Kaskazini na baadaye Juni 6, 2016, Angola aliteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri kama Waziri wa Ulinzi akichukua nafasi ya Jenerali Jeje Odongo, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Ndani ya Baraza la Mawaziri.

Umauti

Asubuhi ya Mei 2, 2023 majira ya saa mbili asubuhi umauti ulimkuta baada ya kupigwa risasi na mlinzi wake akiwa nyumbani kwake Kyanja jijini Kampala

Msemaji wa Polisi, Fred Enanga amewaambia waandishi wa habari mjini Kampala kuwa Engola alipigwa risasi alipokuwa akiingia kwenye gari yake kwenda kazini.

"Alipigwa risasi nyumbani kwake Kyanja na mlinzi wake mmoja ambaye inadaiwa alifyatua risasi kadhaa akiwa karibu. Alikimbia kutoka eneo la tukio hadi kituo cha biashara cha Kyanja, Ring Road ambako aliingia saluni na pia kujipiga risasi," ameeleza Enanga.

Taarifa ya Polisi inasema muuaji ametambuliwa kwa jina la Pte Wilson Sabiti, ambaye naye amejipiga risasi baada ya kutekeleza mauaji hayo, kwa mujibu wa tovuti ya Daily Monitor ya nchini Uganda.

Naye msaidizi wa Waziri aitwaye Ronald Otim pia amepata majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya Mulago kwa matibabu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live