Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meli ya kwanza kubwa ya DRC yatia nanga Kigoma

98d48bb4b24a1f3fd8cb9315979e71bd Meli ya kwanza kubwa ya DRC yatia nanga Kigoma

Tue, 27 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MELI ya Mv Amani inayomilikiwa na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) imekuwa meli ya kwanza kubwa ya abiria kuanza kutoa huduma katika ziwa Tanganyika katika karne hii ya 21.

Uwepo wa meli hiyo umeelezwa utatoa fursa kubwa ya kibiashara na kukuza uchumi kwa nchi zinazounganishwa na ziwa Tanganyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Amani International Investment, Solomon Nasuma akizungumza katika hafla fupi ya mapokezi ya meli hiyo kwenye bandari ya Kigoma alisema meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 600 kwa wakati mmoja ikiwa na vyumba 22 vya kulala.

Aidha meli hiyo ina uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 350 na kubeba magari 50 kwa wakati mmoja huku ikitumia saa nne kutoka Kalemie jimbo la Kivu ya kusini hadi bandari ya Kigoma tofauti na meli na boti nyingine ambazo zimekuwa zikitumia saa 12.

"Tumeona ipo fursa kubwa ya kibiashara katika usafiri wa majini, hivyo tumeamua kuanzisha safari za meli kwa ujenzi wa meli hii kubwa kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa nchi zinazounganishwa na ziwa Tanganyika," alisema Nasuma.

Akizungumza baada ya kupokea meli hiyo Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema hiyo ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa nchi za Burundi, Zambia, DRC na Tanzania kutumia usafiri huo kukuza biashara zao ambazo ni faida kubwa kwa nchi zao.

Andengenye alisema kuwa wafanyabiashara hao wa DRC wametangulia wakati Serikali ya Tanzania ikiwa mbioni kuleta meli mbili kubwa kwa ajili ya abiria na mizigo na kwamba pamoja na kuanza safari kwa meli hiyo bado fursa ya uwekezaji kwa usafirishaji majini ziwa Tanganyika ni kubwa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa Kigoma, Juma Chaurembo alisema kuanza safari kwa meli hiyo kunatoa uhakika wa wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kwa hali ya usalama ulinganisha na usafirishaji wa kutumia boti ambao ulikuwa na mashaka.

Chanzo: habarileo.co.tz