Meli ya kivita ya Urusi iliyojihami kwa silaha za hypersonic zinazozidi kasi ya sauti mara tano zitashiriki katika mazoezi ya pamoja na wanajeshi wa majini wa China na Afrika Kusini mwezi Februari, shirika la habari la serikali la Urusi la Tass linaripoti likinukuu chanzo cha kijeshi.
"Meli hiyo itakuwa katika kituo cha usafirishaji katika bandari ya Syria ya Tartus, na baada ya hapo itashiriki katika mazoezi ya pamoja na wanamaji wa China na Afrika Kusini," shirika hilo linaripoti.
Ilikuwa mara ya kwanza kutajwa rasmi kwa ushiriki wa meli hiyo ya kivita, ambayo ina silaha za makombora ya Zircon, shirika la habari la Reuters linaongeza.
Siku ya Alhamisi jeshi la Afrika Kusini lilitangaza mwezi ujao kuwa litafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Urusi na China katika pwani yake.
Mazoezi hayo yatafanyika kwa siku 10 kuanzia tarehe 17 Februari hadi 27 Februari katika mji wa bandari wa Durban na Richards Bay.
Lengo ni kubadilishana ujuzi na maarifa ya kiutendaji, Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini lilisema.