Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi ya Namungo yafutwa

55b390cac61b3318629067315fe69e9a Mechi ya Namungo yafutwa

Sun, 14 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefuta mechi kati ya CD de Agosto na Namungo FC uliokuwa huchezwe kwenye Uwanja wa 11 de Novembro kuanzia saa 1:00 usiku leo.

Namungo waliwasili Angola juzi kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji hao na kuwekwa chini ya ulinzi kwa madai kuwa kuna viongozi na wachezaji wanashukiwa kuwa na virusi vya corona.

Akizungumza na gazeti hili Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Cliford Ndimbo alisema mamlaka nchini Angola zilitaka timu nzima ya Namungo iwekwe katika karantini baada ya kuwasili nchini humo juzi na kufanyiwa vipimo vya corona.

“Kutokana na kadhia hiyo CAF imesema suala kuhusu mechi hiyo litafikishwa katika kamati husika kwa ajili ya uamuzi,” alisema Ndimbo.

Awali, Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu alisema tangu juzi walisumbuliwa kwa kisingizio cha corona.

“Baada ya hapo wakataka kutuweka karantini tukakataa kwa sababu sisi hatuna maambukizi. Wakaja askari wanajeshi wasiopungua 60 wakatulazimisha kuingia kwenye basi wakatuambia wanatupeleka hoteli ambayo serikali imelipia.”

“Wametutoa mjini tumetembea umbali wa saa 2:30 tupo nje kabisa ya mji. Tumeletwa kwenye hospitali ya jeshi timu tunayokwenda kucheza nayo ni ya jeshi,”alisema.

Alisema baada ya kufika hospitalini waliwalazimisha kuingia kila mmoja kwenye chumba chake wakae huko kwa muda wa siku tatu ila wao walikataa kushuka kwenye basi askari wakaamuru basi walilopanda lifungwe wakaondoka.

Zidadu alisema wanaodaiwa kukutwa na corona ni wachezaji watatu Lucas Kikoti, Fred Tangalu, Hamisi Mgunya na Mkurugenzi Mtendaji wa Namungo, Omary Kaya.

Mwenyekiti huyo alisema walijaribu kuzungumza nao ili wawaruhusu kurudi Tanzania lakini walikataa na wote walinyang’anywa hati zao za kusafiria.

Awali mapema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiahirisha bunge jana alisema yaliyowakutana Namungo ni sehemu ya siasa za mpira wa Afrika na kusema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania inafuatilia ili waachwe.

“Namungo inashikiliwa na jeshi la Angola na hizo ni siasa za mpira Afrika na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania inaendelea kushughulikia ili timu hiyo iweze kushiriki mchezo na kurejea nyumbani,” alisema.

Kwa upande wake TFF nayo mapema jana ilisema inafuatilia taarifa kuwa timu ya Namungo FC imekumbwa na kadhia nchini Angola kwa kutakiwa kuwekwa karatini na mamlaka za nchi hiyo.

Kitendo cha timu hiyo kushikiliwa huko Angola kiliwahuzunisha wapenzi wa soka nchini na kulaani na kuomba mamlaka husika kuchukua hatua kali kwana kinarudisha nyuma soka Afrika.

Chanzo: habarileo.co.tz