Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchungaji Makenzi na wenzake kusalia rumande kwa siku 30 zaidi

Makenzie 741582 Mchungaji Makenzi na wenzake kusalia rumande kwa siku 30 zaidi

Tue, 19 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama mjini Mombasa nchini Kenya, imeagiza kuendelea kuzuiliwa kwa siku 30 zaidi, mchungaji mwenye utata, Paul Makenzi na wafuasi wake 28 ili kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi kuhusiana na kesi ya mauaji ya Shakahola kabla ya kutoa uamuzi kuhusu ikiwa wadhaminiwe.

Makenzi kwa mara ya kwanza alikamatwa April 15 mwaka huu akituhumiwa kuwashawishi wafuasi wake kufunga kula hadi kufa kwa madai wataharakisha kufika mbinguni.

Aidha anatuhumiwa kutumia dini kueneza itikadi kali kwa wanachama wake, ambao baadhi walikataa kusoma na hata kupatiwa matibabu ya hospitali, ambapo tangu kukamatwa kwake miili ya watu 429 ilipatikana katika msitu wa shakahola.

Hadi sasa Makenzi amekuwa rumande kwa karibu miezi mitano bila kushtakiwa, ambapo wiki iliyopita wafuasi wake wengine waliagizwa kuzuiliwa kwa siku 30 zaidi kupisha uchunguzi, ambapo wote wameomba kupewa dhamana.

Wote hawa wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwemo, mauaji, ugaidi, kusaidia watu kujiua, utekaji, mauaji, ukatili dhidi ya watoto na utakatishaji fedha.

Akizungumza katika mahakama ya Shanzu hapa Mombasa, afisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Jami Yamina alisema licha ya kuzuiliwa kwa Mackenzie kwa zaidi ya miezi mitano, polisi hawajahitimisha uchunguzi wao kuhusu vifo vya zaidi ya watu 429 katika msitu wa Shakahola.

Wakili wa Mackenzie, Wycliff Makasembo aliomba kuongezewa muda wa wiki mbili ili kupitia maombi mapya na kuwasilisha majibu. Alitaja kuwa alikuwa mwathirika wa tukio la uporaji siku ya Jumapili usiku, ambalo lilimwacha na majeraha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live