Staa wa muziki kutoka Nigeria, David Adedeji Adeleke maarufu Davido amewataka watu kutulia nyumbani ili kupambana na kuenea kwa virusi vya corona (COVID-19).
Mkali huyo wa wimbo ‘Sweet in the middle’ ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram, mara baada ya kueleza jinsi mchumba wake Chioma Rowland alivyopata maambukizi ya virusi vya corona.
“Tulia nyumbani, hatua hiyo itasaidia kupunguza kuenea kwa virusi hivi, kwa pamoja tunaweza kuimaliza corona,” ameandika Davido.
Awali, mmiliki huyo wa wimbo ‘Owo Ni Koko’, ameeleza mchumba wake huyo alivyopata maambukizi ya virusi hivyo baada ya kuchukuliwa vipimo Machi 25,2020.
Staa huyo ameeleza hivi karibuni alirudi kutoka Marekani ambako aliahirisha ziara ya kimuziki na mchumba wake aliyekuwa London nchini Uingereza naye alirudi pia.
Kutokana na historia ya safari zao, waliamua kupima ili kubainika kama wamepata maambukizi au la, baada ya vipimo vilivyohusisha watu 31 akiwamo mtoto wao, majibu yalionyesha Chioma amepata maambuzki.
Pia Soma
- Kolabo za nje zinavyombeba Diamond Platnumz kimataifa
- Diamond Platnumz afikisha watazamaji milioni 900 Youtube
- Harmonize aanza maajabu kupitia Afroeast2020
“Yupo katika uangalizi ingawa hana dalili yoyote, mimi pia nimejitenga kwa siku 14 ili kujisikilizia” ameandika Davido.
Davido amewashukuru mashabiki wake na kumsihi kila mmoja kukaa nyumbani kwani hatua hiyo itasaidia kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.